KIKOSI cha Taifa Stars kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi ya marudiano ya kuwania fainali za michuano ya Mabingwa wa Afrika (CHAN) dhidi ya Sudan, huku yakitengenezwa mazingira ya kuwamaliza Wasudani walioshinda mechi ya kwanza kwa bao 1-0.
Stars ilifungwa bao katika mechi iliyopigwa wikiendi iliyppita huko Mauritania ikiwa ni mchezo wa raundi ya kwanza na Jumapili hii inahitaji kushinda ili isonge mbele licha ya kuwa na uhakika wa kuwa wenyeji wa fainali hizo za mwakani zitakazofanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Katika kuhakikisha Stars inawazima Wasudani, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeupeleka mchezo huo, Uwanja wa Azam Complex na kuruhusu mashabiki kuingia buire uwanjani kuishangilia timu hiyo mwanzo mwisho kuwahamasisha wachezaji.
Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amefafanua umuhimu wa Taifa Stars kupigania nafasi yake kimchezo.
“Pamoja na kwamba tayari tunayo nafasi kama wenyeji, lakini kwetu ni muhimu kufuzu kwa kushinda ili kujiweka katika kundi la kwanza na kuweza kukwepa timu ngumu,” alisema Ndimbo, aliyefafanua kikosi kipoa tayari kwa mchezo huo wa marudiano.
Katika mchezo wa awali dhidi ya Sudan uliofanyika Mauritania, Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0. Hii ina maana kuwa Stars inahitaji ushindi wa angalau mabao 2-0 ili kufuzu moja kwa moja.
Wakati Stars wakiwa kwenye maandalizi ya hali ya juu kuhakikisha wanapata matokeo mazuri. Kikosi hicho kinaamini kuwa nguvu ya mashabiki na ari ya kuwa nyumbani itawaongezea morali na kuisaidia timu kuvuka hatua hii muhimu.
Mechi hii itakuwa bure kwa mashabiki, hivyo TFF imewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kutoa sapoti kwa Taifa Stars.