Tishio magonjwa yasiyoambukiza yakiongezeka Tanzania

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ‘NCDs Week’ takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR), zinaonesha asilimia 71 ya vifo vyote duniani vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza.

Magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani, kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa kinywa na meno, masikio pua na koo na magonjwa sugu ya mapafu, yametajwa kusababishwa na utumiaji wa tumbaku, kutofanya mazoezi ya mwili, matumizi mabaya ya pombe, milo isiyofaa na uchafuzi wa hewa.

Tunapoadhimisha wiki hii yenye kaulimbiu ‘Time to Lead’ janga la magonjwa yasiyoambukiza huleta matokeo hasi ya kiuchumi na kiafya kwa watu binafsi, familia na jamii yakitishia kulemea mifumo ya afya.

Dhamira ya WHO ni kutoa uongozi na msingi wa ushahidi wa hatua za kimataifa kuhusu ufuatiliaji, kuzuia na udhibiti wa NCDs. Hatua za haraka za serikali zinahitajika ili kufikia malengo ya kimataifa ili kupunguza mzigo wa magonjwa haya.

Mwaka 2016 vifo milioni 41 sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani vilitokana na magonjwa haya na asilimia 75 ya vifo vyote vinavyohusu watu wenye miaka 30 hadi 70 husababishwa na magonjwa haya.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, magonjwa haya yanaongezeka kwa kasi na kuwaathiri hasa watu wenye umri mdogo wakiwemo watoto.

Tafiti za miaka ya 1986/1987 zilionesha mtu mmoja pekee alikuwa na kisukari, watano shinikizo la damu.

Daktari bingwa na mbobezi wa magonjwa ya kisukari, Profesa Andrew Swai anaeleza hali ilivyokuwa hapo awali na hali ilivyo sasa nchini.

Profesa Swai ambaye ni daktari mkongwe eneo la magonjwa yasiyoambukiza anasema mwaka 1976 ndipo ilianzishwa kliniki ya kwanza ya wagonjwa wa kisukari kwa kuwa Tanzania nzima hilo tatizo halikuwepo.

“Ilipofika mwaka 1986 tulifanya utafiti uliobaini wagonjwa wa kisukari walikuwa ni Dar es Salaam, Morogoro, Bahi na Mara. Kwa wakati huo ni asilimia moja tu ya watu ndiyo waliokuwa na ugonjwa wa kisukari na asilimia 5 pekee shinikizo la damu na asilimia 5 ya watu wazima ndiyo waliokuwa na unene uliozidi,” anasema.

Profesa Swai aliyetibu na kufundisha madaktari wengi hapa nchini, anasema tafiti zinazoendelea kufanyika nchini zinaonyesha ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo saratani.

“Zamani tulikuwa na Ocean Road inayotibu magonjwa mengi, ongezeko la wagonjwa wa saratani likatufanya tuiache itibu saratani pekee,” anafafanua.

Profesa Swai ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) anasema maisha ya Watanzania yamebadilika hatua kwa hatua na kusababisha ongezeko hilo.

“Zamani chumvi tulitumia kidogo sana, mama yangu alikuwa akinituma kuchota maji na kutafuta kuni nikitoka shule, leo watoto wanachukuliwa na basi na kurejeshwa hivyo hivyo hawatembei kufanya mazoezi.

“Hakukuwa na juisi tulikula matunda yenyewe na nyuzinyuzi zake, tulikula dona au sembe zilivyo, leo tunakula maandazi yamejaa mafuta, kuku wana mafuta, tunakunywa bia badala ya mbege.

“Tuliishi kijamaa, tulilima pamoja na kutembea pamoja leo tunatumia bodaboda kila mahali, simu janja zinaondoa kushirikiana ndani ya familia hatuzungumzi, hatutembeleani imechangia wengi kupata msongo sasa magonjwa ya akili yanakuja juu,” anasema Profesa Swai.

Elimu na uchunguzi umekua ukitolewa mara kwa mara kwa jamii. Hata hivyo miongoni mwa mambo yanayosababisha magonjwa yasiyoambukiza hasa moyo na ubongo ni kutozingatia afya kinywa na meno.

Tabibu wa kinywa na meno, Lilian Pesha anasema kuna uhusiano wa moja kwa moja wa jino na afya ya ubongo na moyo, hivyo kutotunza afya ya kinywa na meno kunaweza kuchagiza magonjwa hayo.

“Kama mtu anaumwa jino, labda limetoboka wale wadudu wanatoka kwenye jino wanaingia kwenye fizi wakishaingia wanatengeneza maambukizi, unatoka usaha ambao wakati mwingine unashuka na maumivu makali mpaka kwenye mishipa ya damu inayokwenda moja kwa moja kwenye moyo,” anasema.

Pesha anayetoa huduma katika mradi wa ‘NCD Awareness’ kupitia kambi za afya za Vodacom Tanzania Foundation anashauri wenye matatizo ya meno kusaka tiba za mapema kuepuka athari za magonjwa yasiyoambukiza.

“Meno ya chini mawasiliano yake yapo kwenye moyo, ya juu kwenye ubongo na ndiyo maana wakati mwingine mgonjwa akiwa na matatizo ya moyo akaugua jino ukimchoma ile ganzi inashtua moyo mapigo yanaenda mbio,” anasema.

Mtaalamu wa masikio pua na koo ambaye ni mkuu wa kambi hiyo, Dk Adam Sijaona anasema kuna mwamko mdogo wa watu kupima magonjwa yasiyoambukiza lakini pia kufuata mtindo bora wa maisha.

“Maambukizi ya masikio ni tatizo tumeliona Biharamulo, ikifuatiwa na upotevu wa usikivu pamoja na shida ya koo. Watoto zaidi mfumo wa pua na koo,” anasema.

Dk Sijaona anasema shida kubwa waliyoiona ni shinikizo la damu na kwamba asilimia 50 ya wanaofuata matibabu katika kambi hiyo wana shinikizo la damu.

Meneja Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald anasema kambi hiyo ililenga kuwekeza katika elimu na afya kwa jamii na magonjwa yasioambukiza yakipewa kipaumbele, hivyo wanawafikia wananchi kupitia uchunguzi, matibabu na dawa bure.

Pamoja na hayo, Sandra aliongeza kuwa kwa mara ya kwanza mwaka huu, afya ya akili imepewa kipaumbele ikiwa ni hatua mojawapo ya kupambana na athari zitokanazo na matatizo ya afya ya akili ambayo yanaweza kuepukika.

“Kwa muda wa wiki tatu tunahakikisha wananchi wanapata elimu na huduma hasa tunalenga wale wasio na uwezo wa kuzifikia huduma, tangu mwaka jana tunafanya kambi hii katika wiki ya magonjwa yasiyoambukiza tukiungana na wadau wengine huku tukishirikiana na serikali” anasema.

Sandra anasema kambi hiyo wameifanya katika mikoa minne, Dodoma, Singida, Kagera (Biharamulo) na Geita (Chato) wakiwa na madaktari wataalamu wa magonjwa ya meno, koo masikio, pua, kisukari na uchunguzi wa saratani huku akiongeza kwamba kambi hizi ni endelevu.

Takwimu za Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (Mtuha) zinaonesha ongezeko la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka 2,626,107 waliotibiwa mwaka 2019 ikilinganishwa na wagonjwa 3,140,067 mwaka 2023, hii sawa na ongezeko la wagonjwa 513,960 sawa na asilimia 20 ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Meneja wa Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu anataja magonjwa yaliyosababisha wengi kuhudhuria vituo vya afya ni pamoja na shinikizo la damu kutoka 1,112,704 mwaka 2019 hadi 1,482,911 mwaka 2023 na kisukari 464,110 mwaka 2019 hadi 674,399.

“Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu unachangia kwa zaidi ya asilimia 47 ukifuatiwa na ugonjwa kisukari kwa asilimia 21 ya wagonjwa wote wanaopatiwa huduma kwenye vituo vya afya,” anasema.

Dk Ubuguyu anasema magonjwa hayo mawili ndiyo chanzo kikuu cha ongezeko la magonjwa mengine mengi kama vile tatizo la figo, uoni pamoja na kiharusi.

Aidha taarifa za MTUHA zinaonesha mwaka wa 2021 ugonjwa wa pneumonia ukiongoza kuchangia vifo kwa asilimia 19.5, ukifuatiwa na ugonjwa wa moyo kwa asilimia 4.5, shinikizo la juu la damu ikichangia kwa asilimia 3.8 na ugonjwa wa kisukari ukishika nafasi ya tisa kwa kuchangia asilimia 2.5 ya vifo.

“Hali hii inaonesha magonjwa yasiyoambukiza yasipodhibitiwa yanaweza kusababisha ongezeko la vifo nchini,” anasema.

Akitaja taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa katika jamii, Dk Ubuguyu anasema takwimu za WHO kwa mwaka 2022, Tanzania iliripotiwa kuwa na jumla ya wagonjwa wapya wa saratani takribani 44,931 wanaogundulika katika maeneo mbalimbali kila mwaka na vifo 29,743 huripotiwa.

Anasema takwimu hizi zinaonesha saratani tano zinazoongoza nchini ni pamoja na saratani ya mlango wa kizazi kwa asilimia 24.1 ikifuatiwa na tezi dume (10) matiti (9.1) koo (7.9) na Saratani ya Utumbo mpana (4.9).

“Saratani zinazoathiri wanawake hususani saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti kwa pamoja zinaathiri takribani theluthi moja sawa na asilimia 33.1 ya wagonjwa wote, hii ikimaanisha katika kila watu watatu wenye saratani, mmoja atakuwa na kati ya saratani hizi mbili,” anafafanua.

Pia anataja ugonjwa wa selimundu na kwamba takwimu zinaonesha asilimia 15 hadi 20.3 ya Watanzania wanaishi na vinasaba vya ugonjwa huo na hivyo kuwa na uhatarishi mkubwa wa ugonjwa kuendelea kwa kasi hapa nchini.

“Asilimia 0.8 hadi 1.2 ya watoto wanaozaliwa nchini huzaliwa na ugonjwa huu sawa na 14,000 hadi 20,000 kwa mwaka na endapo hakuna huduma zinazotolewa asilimia 70 hadi 90 wanaweza kufariki kabla hawajatimiza miaka mitano.

“Kwa sasa kuna jumla ya vifo 10,742 vya watoto chini ya miaka 5 vinavyotokana na ugonjwa huu,” anasema.

Dk Ubuguyu anasema taarifa ya MTUHA inaonesha changamoto za wasiwasi na sonona ndizo zinazoonekana zaidi.

“Taarifa zinaonesha kuna wagonjwa wa afya ya akili wapatao 390,883 walioonwa katika vituo vya kutolea huduma kwa mwaka 2023,” anasema.

Aidha, mikoa yenye idadi kubwa ya mahudhurio ya wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili nchini ni pamoja na Dar es salaam asilimia 21, Morogoro (6.8) Tanga (6.7) na Dodoma (6.7) wakati mikoa iliyokuwa na idadi ndogo ya mahudhurio ni pamoja na Katavi (0.4), Simiyu (0.6), Rukwa (0.8), Songwe (1.1) na Shinyanga (1.4).

Kwa mujibu wa Dk Ubuguyu hadi kufikia Desemba, 2023 jumla ya watumishi 2,890 kutoka halmashauri zote 184 na vituo vya afya vya umma 711 wamejengewa uwezo katika kutoa huduma za magonjwa yasiyoambukiza.

Pia wamewezeshwa kupata vitendea kazi ikiwemo mashine za kupima shinikizo la damu, kupima sukari, vifaa vya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na vifaa vingine vya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kwenye ngazi ya msingi.

Lengo la uwekezaji huu kwenye ngazi ya jamii ni kuwezesha watoa huduma waweze kutoa elimu na kusaidia jamii kuzuia magonjwa yasiyoambukiza, kuwezesha vituo vya afya kufanya uchunguzi wa hali ya afya na kutoa huduma mapema ili kuzuia madhara yatokanayo na magonjwa yasiyoambukiza.

Kliniki hizi zinawezeshwa kwa ajili ya kutoa huduma za kisukari, saratani, shinikizo la juu la damu, afya ya akili na huduma za macho na utengamao.

Pia mafunzo kwa watoa huduma 162 kutoka katika vituo vya kutolea huduma 16 vinavyotoa huduma za afya ya akili na dawa za kulevya. Vituo hivi vimeteuliwa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa na ongezeko la mahitaji kwenye maeneo ya huduma.

Related Posts