Ukweli kuhusu ute na ulaji bamia

Mmoja wa wasomaji (jina limehifadhiwa) alieleza ameacha kununua mboga aina ya bamia kutokana na dhihaka aliyokutana nayo sokoni.

Alieleza kuwa aliwasikia watu wakisema wanawake hununua mboga hiyo ili kuongeza ute katika maeneo ya uzazi. Hivyo, aliamua kuuliza swali kama kuna ukweli wowote kuhusiana na hilo. Jibu kwa kifupi, sio kweli ni potofu.

Ukweli ni kuwa makundi saba ya vyakula tunavyokula vikisheheni virutubisho, madini na vitamini mbalimbali ambazo zinatumiwa na seli za mwili katika kazi mbalimbali, ikiwamo kutengeneza maji maji ya mwilini.

Mwonekano wa mboga hiyo wakati wa kula, haina maana kuwa itafika kama ilivyo ambavyo baadhi hudhani. Tunapokula vyakula hufika katika mfumo wa chakula na kuvunjwa vunjwa.

Ingawa ni kweli bamia ni jamii ya mboga majani yenye virutubisho, vitamini na madini ambavyo vinasaidia mambo mbalimbali, ikiwamo kutengeneza maji maji mwilini, lakini si kula bamia pekee itaongeza ute au majimaji eneo la uzazi.

Hii ni kwa sababu mwili hauwezi kufyonza vyakula tunavyokula kama vilivyo, ila ni mpaka baada ya kusagwa na kuchakatwa hatimaye kuwa katika hali ndogo kabisa.

Ute maeneo ya uzazi, mdomoni, mfumo wa hewa na chakula hutengenezwa na kuzalishwa na seli hai maalumu ambazo huwepo maeneo mbalimbali, ikiwamo katika tezi maalumu zinazozalisha majimaji.

Kila ute unaotengenezwa na mwili una kazi yake maalumu kutokana na eneo uliopo. Mfano njia ya hewa kazi yake kudaka vitu vinavyoingia katika njia ya hewa.

Vile vile kusafisha njia ya uzazi kila siku kwa kusomba seli zilizokufa pamoja na mabaki mengine yasiyohitajika. Hali hii ni mchakato wa asili kwa eneo kuwa safi, hatimaye afya njema. Ndiyo maana wataalamu wa afya kwa kinamama hushauri kutoingiza kitu ukeni ili kusafisha eneo hilo.

Vile vile ute huo ni kilainishi asili kinachowezesha mtoto kusafiri salama wakati wa kuzaliwa na pia wakati wa tendo, ili kuleta msisimko.

Kiwango cha ute njia ya uzazi hutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine, hii ni kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo magonjwa, uvimbe na kuyumba kwa vichochezi.

Utokaji wa ute wenye afya ni ule usio na rangi au kwa mbali kama maziwa na inaweza kuwa na harufu kidogo isiyo mbaya ya kukera.

Hubadilika pia katika kipindi cha mzunguko wa hedhi wa mwanamke, ikiwamo kuwa na rangi na unene. Mabadiliko mengine inaweza isiwe ya kawaida, hivyo kutoka au kutotoka kunaweza kuonyesha ni dalili ya ugonjwa.

Kabla na wakati wa kupevuka kwa kijiyai cha kike yaani ‘ovulation’ ni kawaida kwa ute eneo la uzazi kuongezeka, ute huo huwa mzito kama vile wa yai bichi ambao huvutika bila kukatika ukishikwa kwa vidole viwili.

Mwili ulio na afya unahitaji vitamin A, B, E, beta carotene na mafuta ya tindikali ya omega-3 ili kuongeza kiwango cha ute mwilini. Bamia lina beta corotene, lakini halina vitu hivyo hapo vyote. Vile vile bamia lina virutubisho, vitamini K, antioxidant na madini kama vile chuma na kalisiamu.

Vyakula vyenye mafuta ya omega 3 ni samaki, vitamini A inapatikana katika mboga za majani kama mchicha, bamia, wakati vitamini B kama vile nyama, mayai, maziwa na mazao yake na baadhi ya nafaka.

Wakati beta carotene ni kirutubisho ambacho mwili hukibadili na kuwa vitamini A, hupatikana zaidi kwenye matunda yenye njano kama vile machungwa, karoti na nyanya na mboga majani.

Ni muhimu kufika huduma za afya kwa ushauri sahihi na matibabu. Zingatia lishe bora mchanganyiko, ila ulaji matunda na mboga kwa wingi una faidi nyingi kiafya.

Related Posts