Vijana kupenda ‘mashangazi’…Tatizo linaanzia hapa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kuagiza ufanyike utafiti kubaini mzizi wa vijana wa kiume kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na wanawake wanaowazidi umri maarufu mashangazi, wadau na viongozi wa dini wameeleza kiini cha tatizo hilo kuwa ni mfumo wa malezi.

Sambamba na hilo, wamesema endapo hatua stahiki hazitachukuliwa kudhibiti mwenendo huo, utawafanya vijana kuwa tegemezi.

Oktoba 21 akiwa katika mkutano wa kitaifa wa utafiti na maendeleo, Dk Mpango aligusia suala la maadili na kueleza namna anavyosikitishwa na idadi ya vijana wanaoingia kwenye uhusiano na mashangazi inavyoongezeka.

Akizungumza na Mwananchi jana, Askofu Jackson Sostenes wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, alisema changamoto kubwa ipo kwenye malezi.

Alisema vijana wengi wanakua kwenye familia wakishuhudia majukumu ya kulea familia yakibebwa na mama.

“Hii mada nimeitoa kwenye mahubiri Jumapili, sasa hivi wazazi wanashindwa kuwasaidia vijana kujitambua. Kijana anashuhudia mama yake akifanya kila kitu, kichwani mwake anatengeneza picha, kuwa hivi ndivyo inavyopaswa kuwa,” alisema.

Alisema karibu asilimia 65 ya familia hivi sasa mzigo wa kulea familia unabebwa na wanawake na ndiyo maana wengi wao wanajiunga na Vicoba, wanaingia kwenye mikopo ikiwemo ya kausha damu lengo likiwa kutafuta kipato. “Wanaume wamebweteka, sasa mtoto wa kiume akiona vile anaamini kwamba na yeye anastahili kulelewa,” alisema askofu Sosteness.

Alisema matokeo ya hilo ni jamii kuwa na watu wengi wenye jinsi ya kiume lakini si wanaume kwa kuwa wanashindwa kubeba majukumu wanayostahili kuyabeba wanaume.

Askofu huyo anatahadharisha kuwa hali ikiendelea hivi itafika wakati wanaume hawatakuwa na nafasi kwenye jamii badala yake watabaki kama wachangia mbegu za kuzalisha watoto.

Mtazamo wa askofu huyo unaendana na mawazo ya Dk Katanta Simwanza, mwanzilishi wa jukwaa la Tanzania Boys & Men’s Ambassadors (TBMA).

Simwanza alisema changamoto inaanzia kwenye malezi kutokana na wazazi kutotimiza majukumu yao ipasavyo, hivyo watoto wanashindwa kujua mipaka ya vitu vya kufanya na wasivyotakiwa kufanya.

Alisema hali hiyo inawafanya vijana kuangukia kwenye tabia za hovyo ikiwamo kupenda starehe na anasa ilhali hawana kipato, hivyo kimbilio lao linakuwa kwa wanawake watu wazima.

“Hatari ya hii inatuondoa kwenye ule utamaduni wa kawaida wa mwanaume kuwa kichwa, kwa kuwa kwenye uhusiano wa aina hii mwanamke ni mkubwa kiumri na inawezekana ana fedha basi yeye ndiye anakuwa na mamlaka na mfanya maamuzi.

“Kama hivyo ndivyo, huenda mwanamke huyu akambana kijana na asimpe fursa ya kufanya vitu vingine, hapo ataendelea kuwa tegemezi na atatumia muda wake mwingi kutafuta namna ya kumridhisha mfadhili wake,” alisema Dk Simwanza.

Dk Simwanza ambaye ni mtaalamu wa afya, alisema hali hiyo inawafanya vijana wengi kuangukia kwenye changamoto ya afya ya akili na maambukizi ya magonjwa mengine ya zinaa pamoja na Ukimwi.

Alisema, “kwa kuwa kijana huyu hana maamuzi, analazimika kufanya vile anavyotaka huyo ‘shangazi’, sasa hapa ndiyo kuna ngono isiyo salama inayoweza kumsababishia maambukizi ya maradhi.

“Pia tunashuhudia vijana wengi wakitumia muda mwingi kuangalia picha na video za ngono wakijifunza mbinu za kuwaridhisha hao wafadhili wao na hili linawapelekea kwenye changamoto ya afya ya akili,” alisema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, athari hizo hazitaishia kwa kijana pekee, bali familia na Taifa kwa ujumla kutokana na kupoteza nguvu kazi.

“Tunashuhudia jamii ikikosa watu wenye kujiamini na kufanya maamuzi na hatari zaidi ni haya yanapofanywa na wanaume. Mwanaume anapopoteza nafasi ya kuwa kiongozi mbele ya mwanamke, hawezi kuwa sawa kisaikolojia,” alisema Dk Simwanza.

Alisema jambo lingine la hatari ni ongezeko la familia za mzazi mmoja. “Hii inakuja pale kijana huyu anapoamua kuanzisha familia yake akapata mwanamke akaoa na akabarikiwa kupata mtoto, kama ataendelea na tabia za utegemezi, ni rahisi ndoa hiyo kuvunjika.

Alisema jamii inaendelea kuyashuhudia mambo hayo, mwanaume anamtegemea mkewe afanye kila kitu kwenye familia, ikifika mahali yule mwanamke akachoka ndiyo ndoa husambaratika.

Kwa upande wake Sheikh Khamis Mataka alisema mwenendo huo ni matokeo wa mmomonyoko wa maadili unaoendelea katika jamii na changamoto za kisaikolojia wanazokumbana nazo vijana.

Mataka alisema kwa asili kijana ni mtu shujaa anayependa kupambana kwa ajili ya familia na Taifa kwa ujumla na inapotokea akawa anajifikiria yeye binafsi, ndipo changamoto inapoanzia.

“Tunavyofahamu vijana ndiyo wenye maarifa, nguvu na fikra za ubunifu. Kwa maana hiyo, lazima aonyeshe ushujaa wake kwa kupambania familia yake na Taifa, ikitokea kijana anawaza tumbo lake tu, ndiyo hapa tunaona vijana wanaoamini katika kujitoa utu wao ili wapate chochote kitu,” alisema sheikh huyo.

Alisema kutokana na mwenendo huo, ndiyo maana vijana sasa wanalemaa hawawezi kujitafutia, wanakaa wakisubiri kupewa na matokeo ya hilo ni kukosa mchango wao kuanzia kwenye ngazi ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Alisema kama familia na Taifa wasipokuwa makini, kundi hilo litazidi kuangamia kwa kukosa maarifa.

Wakati jamii ikiwatazama hivyo, wamedai changamoto ya ukosefu wa ajira imechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya waingie katika mahusiano hayo kwa sababu za kiuchumi.

Mathayo Kihwelo, muuza mitumba wa Mbagala, Dar es Salaam alisema “hakuna ajira, maisha ya vijana wasomi yamekuwa magumu ndiyo maana ikitokea umependwa na mshangazi unamshikilia kwa sababu wengi wao wana fedha, hivyo wanarahisisha maisha,” alisema Kihwelo.

Kwa upande wake John Marley, mkazi wa Kimara jijini humo, pia alisema, “hapa changamoto ni ajira, hatuna pesa hiyo mishangazi ndiyo tegemeo letu vijana. Serikali itoe ajira sio kutuambia maneno ambayo hayana msaada kwetu.”

Hata hivyo, Jasper Joel, kinyozi katika eneo la Chamazi, alitiofautiana na wenzake, akisema “si wote tunakwenda kwa mashangazi kwa sababu ya hela, wengine hatupendi usumbufu wa hawa wasichana tunaolingana nao umri.

“Unajikuta unahangaika kumpatia kila kitu lakini bado anakusumbua, lakini ukimpata mshangazi hana usumbufu na akifurahishwa na wewe anakupenda sana na anakulea na anakupa mahitaji yako yote.”

Kukabiliana na hilo, Askofu Sosteness alishauri kuwepo jitihada mahususi za kuwabadilisha vijana wa kiume ili warejee kwenye nafasi yao ikiwa ni pamoja na kuwapa fursa zitakazowasaidia kuwaimarisha kiuchumi waondokane na utegemezi.

“Zilifanyika jitihada nyingi za kumuinua mtoto wa kike kwa namna moja au nyingine mtoto wa kiume akasahaulika, sasa tusiangalie tulipoangukia turudi na kuelekeza nguvu hiyo hiyo kwa upande wa pili,” alisema.

Askofu huyo alisema kama ilivyo kwa vijana wa kike kulivyo na fursa nyingi za mikopo, na kwa wakiume nako wapatiwe fursa hizo kwa sababu si kila kijana wa kiume anao uwezo kiuchumi.

Alisema wapo wanaolazimika kufanya mambo yasiyofaa kwa sababu ya hali mbaya ya kiuchumi inayowakabili.

“Zisipofanyika jitihada za aina hii, kuna hatari ya kuwa na jamii na taifa lisilojielewa kwa kuwa nguvu kazi inazidi kuwa tegemezi na wanawake wanabeba mzigo mzito wa kuhudumia familia ambao kwa asili ya Afrika hili ni jukumu la wanaume,” alisema.

Kwa upande wake, Sheikh Mataka alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa dini, wazazi na jamii kwa ujumla kuipinga tabia hiyo inayozidi kuota mizizi kwa kuwa inatengeneza kundi kubwa la utegemezi ilhali walitakiwa kuwa wazalishaji.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts

en English sw Swahili