Dar es Salaam. Ukosefu wa elimu, miundombinu duni, na kukosekana kwa sera bora zimetajwa kuwa changamoto kubwa kwa wanawake katika juhudi zao za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwamo ukame.
Changamoto hizo zinapelekea wanawake wengi kukosa taarifa muhimu kama za mikopo, ambayo ingewasaidia kujiendeleza kiuchumi.
Hayo yamebainishwa Oktoba 31, 2024, katika majadiliano ya siku tatu yaliyowakutanisha wadau na viongozi wa mazingira yaliyoandaliwa na Climatic Hub Tanzania kwa ufadhili wa Women Fund Tanzania (WFT-T).
Mjadala huo ulilenga kuleta usawa wa kijinsia na kuandaa mikakati jumuishi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Miongoni mwa madhara yaliyojadiliwa na wadau hao wa mazingira, ni changamoto zinazowakabili wanawake wanaojihusisha na biashara za mbogamboga na matunda. Ofisa mradi wa Climatic Hub Tanzania, Aron Sanga, amesema wanawake wanaojishughulisha na biashara hizo wanapata hasara hasa katika kipindi cha mvua kutokana na miundombinu duni ya kuhifadhia mazao yao na pia ugumu wa upatikanaji wa bidhaa katika mazingira hayo, hali inayowaathiri kiuchumi.
“Kwa mfano, wanawake wanaouza matunda na mbogamboga wanapata hasara kipindi cha mvua kwa sababu miundombinu si rafiki na pia upatikanaji wa bidhaa hizo unakuwa mgumu, na kufanya wanawake kushuka kiuchumi,” amesema Sanga.
Ameongeza kuwa miundombinu duni ya mawasiliano inawanyima wanawake, hasa wale wa vijijini, huduma za afya ya mama na mtoto katika kipindi cha mafuriko na wakati wanapotafuta huduma hizo.
Aidha, Sanga amebainisha kuwa mjadala huo umeonyesha kuwa wanawake wako hatarini zaidi na wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee katika athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema, “ni dhahiri kuwa hii ni hatua muhimu kuelekea mustakabali jumuishi na endelevu zaidi, ambapo usawa wa kijinsia utatambulika kama sehemu muhimu ya mafanikio katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”
Kwa upande wake, Ofisa Mazingira wa Wilaya ya Kisarawe, Godfrey Ambele, amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kuimarisha vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuwapunguzia mzigo wakulima ili kuwapa moyo katika kukabiliana na mabadiliko haya.
“Upande wa wakulima, Serikali imejitahidi kuwapunguzia mzigo wa makato ili kuwatia moyo katika mapambano ya mabadiliko hayo,” amesema Ambele.