Yaliyofanyika miaka minne ya Dk Mwinyi si haba

Unguja. Wakati Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi anaingia madarakani alijipambanua kujikita katika sera ya uchumi wa buluu na kuunda wizara maalumu itakayosimamia eneo hilo.

Licha ya awali dhana hiyo kutoeleweka kwa wengi na dhamira yake lakini kwa sasa inatajwa kuanza kuleta mabadiliko.

Dk Mwinyi aliapishwa Novemba 2, 2020 kuingia madarakani baada ya kumshinda aliayekuwa mshindani wake wa karibu wakati huo Maalim Seif Sharif Hamad.

Leo anapofikisha miaka minne madarakani sekta hiyo ni miongoni mwa zinazotajwa kufanya vizuri na kuleta mabadiliko.

Kwa takribani wiki nzima, imezinduliwa miradi mbalimbali katika sekta za elimu, uwezeshaji na uwekezaji, huku Rais Mwinyi akihusika kufungua miradi hiyo.

 Akizungumza Novemba Mosi, 2024 wakati wa kufungua Shule ya Sekondari ya Konde, Kaskazini Pemba Rais Mwinyi amesema atawaonyesha watu kwa vitendo na dhamira yake ipo palepale kuibadilisha Zanzibar.

“Wengi walidhani hatutaweza lakini haya tunayofanya ni salamu tosha, tumeahdi tumetekeleza na tutaendelea kutekeleza mengi bado yanakuja,” amesema.

Mawaziri wafunguka mafanikio ya kisekta

Akizungumza mafanikio ya miaka minne katika Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Waziri Shaaban Ali Othman amesema uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa asilimia 110.2 kutoka tani 38,107 zenye thamani ya Sh205.35 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia tani 80,085 zenye thamani ya Sh569.07 bilioni mwaka 2023, huku ukitoa ajira kwa wastani wa watu 63,000 ambao asilimia 17 ni wanawake.

Katika uzalishaji wa mwani, Shaaban anasema umeongezeka kwa asilimia 89.6 kutoka tani 8,785 zenye thamani ya Sh5.387 bilioni hadi kufikia tani 16,653 zenye thamani ya Sh16.5 bilioni na unatoa ajira za moja kwa moja kwa wastani wa watu 16,000, asilimia 80 wakiwa wanawake.

Vifaranga milioni moja vya majongoo bahari vimezalishwa. Kati ya hivyo, 22,000 vimegawiwa kwa wafugaji 310 ambapo Unguja ni vifaranga 7,000 na Pemba 15,000.

“Tumegawa boti za uvuvi na mwani 1,027, Unguja ni 385 na Pemba 642, ambazo zimenufaisha wananchi 32,000, kati ya hao asilimia 70 ni vijana na asilimia 90 ya boti za ukulima wa mwani wanufaika ni wanawake,” alisema Shaaban.

Amesema wamejenga na kugawa mashamba 100 ya kufugia majongoo bahari, mashamba 60 kwa ufugaji wa kaa na mashamba 20 ya ufugaji wa samaki.

“Jumla ya wakulima 1,001 Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo juu ya ukulima wa mwani katika kina kirefu kwa kutumia njia ya kamatia chini na vifaa vya kulimia mwani kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwani Zanzibar (Zasco)” amesema.

Kuhusu mapato yatokanyo na tozo katika sekta ya uvuvi, amesema yameongezeka kwa asilimia 262.5 kutoka Sh1.65 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh6 bilioni mwaka 2023. 

Akizungumza baada ya kupokea data za mafuta na gesi asilia za maeneo ya Zanzibar kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania, amesema  wametangaza na kusimamia duru ya kwanza ya utoaji wa vitalu vinane vya mafuta na gesi asilia baharini kwa ajili ya uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

Amesema umezinduliwa utangazaji wa vitalu viwili vya mafuta na gesi asilia vya nchi kavu kwa ajili ya uwekezaji na ujenzi wa kituo cha muda cha uhifadhi na usimamizi wa taarifa za mafuta na gesi asilia.

“Tumewalipa fidia wananchi 3,577 walioathirika na mtetemo kati ya wananchi 4,330 sawa na asilimia 83, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) inaendelea na hatua za ukamilishaji wa asilimia 17 ya wananchi iliyobakia katika ulipaji wa fidia kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Ndani ya kipindi hicho amesema limejengwa soko na diko (barafu) la kisasa la samaki katika eneo la Malindi ambalo kwa sasa linahudumia wastani wa watu 10,000 kwa siku na boti 350 za uvuvi.

Amesema Serikali imejenga kiwanda cha kusarifu mwani katika eneo la Chamanagwe, Pemba chenye uwezo wa kuchakata tani 30,000 za mwani mkavu kwa mwaka.

Pia imejenga kiwanda cha kutengeneza chakula cha samaki katika eneo la Kama chenye uwezo wa kuzalisha tani tano za chakula cha samaki kwa siku.

Kwa kipindi cha nyuma, shule za Zanzibar zilikuwa zikifanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa lakini kwa sasa imebadilika huku mikakati kadhaa ikitajwa kuleta maabdiliko hayo ikiwa ni pamoja na Serikali kutoa kipaumbele katika sekta hiyo.

Katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 ya Sh5.18 trilioni, sekta ya elimu imepangiwa bajeti ya Sh830 bilioni ikiwa ndiyo sekta inayoongoza kuliko zote.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa amesema bajeti ya maendeleo ya elimu imeongezeka kutoka Sh19 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia Sh518 bilioni mwaka 2024.

“Uandikishaji wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 535,467 mwaka 2020 hadi kufikia wanafunzi 620,609 katika ngazi zote za elimu. Jumla ya watoto 35,941 walirejeshwa shuleni kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita,” amesema.

Amesema ongezeko hilo linatokana na jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule za kisasa katika maeneo yote ya Unguja na Pemba ili kuleta mageuzi katika sekta hiyo.

Amesema madarasa 2,738 yamejengwa na shule za ghorofa 35 kwa kipindi cha miaka minne, huku madarasa mengine mapya 2,037 zikiwemo shule 26 za ghorofa na shule za chini 53  tayari ujenzi wake umeanza kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Pia, zimefanyiwa ukarabati mkubwa shule 91, huku asilimia 67 za msingi na asilimia 87 za sekondari kwa sasa zinaendeshwa kwa mkondo mmoja tofauti na mikondo miwili ya awali.

Akizungumzia suala la ajira,  Lela amesema wizara imeajiri walimu 73 kwa upande wa mahitaji maalumu na kujenga vyuo vya amali vitano Unguja na Pemba ili vijana waweze kujiajiri.

Amesema ufaulu wa wanafunzi wa vipawa na michepuo katika mtihani wa darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 5.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 27,5 mwaka 2023 na ufaulu katika kidato cha pili umeongezeka kutoka asilimia 76.8 hadi kufikia asilimia 94.6, ufaulu katika kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 55.4 hadi kufikia asilimia 85.6 mwaka 2023 na kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 96.2 hadi kufikia asilimia 99.6 mwaka 2024.

Bajeti ya sketa ya elimu imetoka Sh265.5 bilioni mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh830 bilioni mwaka 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 212.6.

Amesema tayari wameajiri walimu 3,600.

Burhan Haji Omar, mdau wa elimu amesema pamoja na mafanikio hayo bado jitihada zaidi zinahitajika ili miundombinu iendane na mabadiliko ya mitalaa kulingana na teknolojia inavyobadilika.

“Changamoto ya elimu yetu siyo tu kwenye miundombinu, lakini elimu inayotolewa inaendana na matakwa ya sasa ya soko la ajira, hili ni jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa kina ili kukimbizana na ulimwengu,” amesema

Related Posts

en English sw Swahili