AKU yaadhimisha Siku ya Waandishi Dar

Dar es Salaam. Serikali imeshauriwa kukusanya takwimu kuhusu idadi ya watu wanaopenda kusoma vitabu ili kuendelea kuhimiza tabia ya usomaji kwa Watanzania.

Takwimu hizo zitasaidia kuimarisha juhudi za kukuza usomaji, kuhakikisha rasilimali zinatumika vyema ili kuhamasisha watu wengi kujenga tabia ya kusoma vitabu na kuboresha matokeo ya elimu nchini.

Wito huo umetolewa jana Ijumaa, Novemba 1, 2024 na wadau wa elimu katika maadhimisho ya Siku ya Waandishi inayoadhimishwa kila Novemba iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU).

Maadhimisho hayo yanawaleta pamoja watafiti, wataalamu na waandishi wa vitabu, machapisho ya elimu na makala kutoka ndani na nje ya nchi.

Mtafiti kutoka taasisi ya utafiti ya ICREA Hispania, Profesa Daniel Brockington, amesema wanapofanya tathmini ya watoto kutoka nchi mbalimbali, utafiti unaonyesha wanaosoma zaidi wapo katika nchi zenye changamoto tofauti na si zile zinazoendelea.

“Kosovo inaongoza duniani kwa hamasa ya usomaji kwa watoto, wakati Norway ni ya mwisho. Afrika Kusini asilimia 50 ya watoto wanapenda kusoma, wakati Uingereza ni asilimia 25 tu wanaopenda kusoma vitabu vya hadithi,” amesema.

Profesa Brockington amesema… “hali hii inazua maswali kwa nini watoto katika nchi zisizoendelea wanaonekana wanasoma zaidi.”

Amesema: “Kama waandishi tunao wajibu mkubwa wa kuwapa vitabu vya kuvutia badala ya kudhani tu kwamba watu hawapendi kusoma, tunapaswa kujiuliza, je, vitabu tunavyoandika vina msisimko wa kutosha kuwahamasisha watoto wengi zaidi kusoma?”

Mkuu wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Aga Khan Tanzania, Jackline Kiwelu, amesema maadhimisho hayo yanazingatia mchango wa watafiti, waandishi na wasomaji.

“Leo tumekusanya wataalamu mbalimbali chini ya kaulimbiu ‘mazingira na mabadiliko ya tabianchi’ kwa sababu wasomaji na waandishi wana jukumu la kuchangia mijadala mingi,” amesema.

Kiwelu amesema kupitia uandishi wa majarida, makala, vitabu vya kiada na aina mbalimbali za maandishi, wanaweza kuhamasisha na kuutarifu umma kuhusu umuhimu wa kusoma vitabu.

Mmoja wa wanafunzi wa AKU, Gladness Nginda amewataka wadau wa elimu katika ngazi mbalimbali kuweka utaratibu wa kuandika na kusoma vitabu ili kushiriki changamoto na kuziwasilisha kwa jamii.

“Kwa njia hii, mawazo yao yanaweza kuleta mabadiliko kama tunavyosema, kichocheo kimoja kinaweza kubadilisha kundi lote,” amesema.

Related Posts