KATIKA sehemu ya kwanza ya simulizi hili la kusikitisha la nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Modest tuliona uhalisia wa mazingira anayoishi nyumbani kwa baba yake mzazi mjini Kigoma na leo kwenye muendelezo anafichua makubwa ikiwamo alivyoanza kuugua. Endelea…
Licha ya mwili wa Modest (juu kitandani) kuanzia shingoni kwenda chini haujiwezi, miguu yake anaweza akaitingisha, lakini haiwezi kusimama wala kufanya chochote. Pamoja na hayo yote bado akili yake imesimama kama kiongozi dhidi ya wadogo zake, kuhakikisha wanakwenda katika njia sahihi, misimamo yake mikali, hapendi kuendeshwa licha ya kuwa kitandani. Kifupi anasimamia kile anachokiamini, bila kujali wengine wanamchukuliaje.
Majina aliyokuwa anaitwa zamani ya mwili nyumba, chuma, pumzi ya moto, yamebakia historia ya kitabu chake cha furaha, kilichofunga kurasa zake huku zikifunguliwa mpya ambazo zina maumivu, yanayomfanya asione sababu ya kuendelea kuwepo duniani.
Kiungo chenye uhakika wa kufanya kazi katika mwili wake ni kichwa pekee, ambacho pia kinatazama juu, hawezi kugeukia upande wa kushoto wala kulia.
Kikubwa anachokifanya ni kuzungumza tu, ingawa kwa mujibu wa ndugu zake kuna wakati mwingine maumivu ya misuli yakimzidia, anakataa kuongea na ndugu zake.
Ikumbukwe mwaka 1998 Yanga iliazima kwa Simba wachezaji watatu ambao ni Monja Liseki, Shaaban Ramadhan na Modest, kuipa sapoti katika hatua ya kutinga makundi, michuano ya CAF.
“Aliyekuwa Rais wa Yanga, Francis Kifukwe, aliwafuata viongozi wa Simba kutuomba wachezaji watatu, ili tukawasaidie kucheza michuano ya CAF ilikuwa ni hatua ya kuingia makundi.
“Kwa nafasi yangu ndani ya Yanga alikuwa anacheza beki mkongwe Kenneth Mkapa ila alikuwa anakwenda kustaafu, ndiyo maana wakanichukua mimi, wote watatu tukawa tunacheza kikosi cha kwanza kwenye michuano hiyo.
“Yanga wapo siriazi sana, baada ya kufika katika klabu yao nikaanza kupewa masharti, hata kwenda dukani ilikuwa ishu, wazee wanakuja wanakwambia sisi ndio Yanga.
“Nakumbuka mechi dhidi ya Asec Mimosas ugenini tukafungwa mabao 2-1, dhidi ya Maning bao 1-1 na Raja Casablanca tukatoka sare ya mabao 3-3 bao la pili nikajifunga kwa bahati mbaya, mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Uhuru.
“Mashabiki wakaanza kusema mtoto wa nyoka ni nyoka, wakimaanisha nimefanya kusudi, baada ya mechi kuisha wakawa wananisubiria nje, kuna mchezaji mwenzangu alisema tubaki vyumbani, tukasubiriwa hadi sasa saba usiku, sasa kuna mmoja wao akasema kwake nakufahamu anaishi Temeke twende tumfuate.
“Wakati anaanza safari rafiki yangu akampigia bodaboda wake akaja akaniwahisha nyumbani, nikafika kabla yao nikafunga geti. Nikiwa ndani nikawasikia nje, wakawa wanaongea hadi muda huu hajarudi (saa 10:00 alfajiri), atakuwa ameenda kufanya umalaya wake tuondoke.”
Anasema kuna timu ilikuwa inamtaka ya Uarabuni, ila viongozi wa Yanga wakamkazia na kutaka asaini mkataba wa kuitumikia katika ligi baada ya mkataba wake na Simba kuisha akagoma na kwenda kumalizana na timu ya Mlandege ya Zanzibar.
“Baada ya kutoka Zanzibar, Mzee Hassan Dalali na Abdallah Kibadeni, wakataka niwasaidie kuwasajilia timu nami nisalie kama mkongwe, nikawatoroka na kwenda Botswana.” Timu aliyoichezea Mbwana Samatta ya KRC GENK, iliwahi kuhitaji huduma yake, Simba haikuwa tayari kumuachia, kama dili lingetiki basi lingekuwa linatajwa jina la Mtanzania, kucheza kabla ya Samatta.
“Kuna kocha mzungu wa timu hiyo, alinikatia tiketi ya ndege, alihitaji barua ya kuniacha huru ili nikasaini mkataba, hilo likawa gumu kwa uongozi wa Simba, hivyo kocha huyo akanishauri niuze tiketi nipate pesa, ikanibidi niuze kuliko kukosa yote.”
ALIVYOUGUA KIMIUJIZA NDOTONI!
Anasimuliwa dalili ya ugonjwa ulivyomuanza, anakumbuka ilikuwa mwaka 2005, kuna usiku mmoja, akiwa amelala aliota ndoto ambayo ikaja kuonyesha uhalisia wake baada ya kuamka asubuhi.
“Kuna siku niliota paka watatu, mmoja alikaa kichwani, mwingine alikaa ubavu wa kushoto na mwingine wa kulia, wakawa wametoa macho makali sana, kisha nyama ilikuwa mbele yangu sikujua ni nyama ya nini.
“Nikawa naamrishwa kula nyama, wakati nagoma wale paka wakawa wanataka kunirarua, nikawa napambana sana, ikanibidi nile ile nyama.
“Niliposhtuka baada ya kula ile nyama ndotoni nikaamka nikajikuta navuja jasho jingi sana, mwenzangu niliyekuwa nimelala naye, akaniuliza umepata shida gani, maana ulikuwa unaweweseka na unatiririka jasho, nikamsimulia ile ndoto. “Wakati nashuka kitandani miguu ikaanza kuniuma sana, nikawa nakanyaga kwa shida, sikuacha kwenda kazini, nikawa nanunua dawa nakunywa, najitahidi kufanya mazoezi na kuchua lakini wapi, nikawa naenda hospitali napata dawa narudi, kuna wakati niliambiwa ute wa kwenye magoti umeisha.
“Kuna siku nikazidiwa nikapelekwa hospitali ya kiwanda cha Mtibwa, baada ya kupimwa nikaonekana nyonga yangu imeachia, wakasema hawawezi kunitibia, ikabidi nipewe rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako nikapolekewa na kufanyiwa vipimo zaidi, ilikuwa mwaka 2018.
“Baada ya kupata matibabu, nakumbuka kuna upasuaji nilitakiwa nifanyiwe ndipo daktari bingwa mmoja wa magonjwa ya mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi-anamtaja) aliniambia usipoteze pesa yako.
“Unapaswa ufanye mazoezi ili nyonga yako iweze kuunga na kwa tatizo lako unaweza ukapata ulemavu wa kudumu.
“Nikawa nafanya mazoezi ndio kwanza hali ikawa inazidi kuwa mbaya, basi nikawaambia ndugu zangu hatuna budi kurudi nyumbani, tukachangiwa nauli nikarejea hapa Kigoma, usione naongea sana,
“Nilikuwa mkimya ninayependa utulivu, ila kwa sasa ugonjwa umenifunza kuongea, maana ninapotembelewa na watu inakuwa ndiyo muda wangu wa kupata faraja, wakiondoka nabakia kimya muda mrefu.”
“Wakati natoka Dar es Salaam, nilikuwa na uwezo wa kukaa kwenye kiti cha walemavu, kujilisha mwenyewe, kadri muda unavyokwenda nikashindwa nipo hapa kitandani zaidi ya miaka mitano, siwezi kila kitu zaidi ya kuongea tu.