KOCHA Mkuu wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge amesema, kitendo cha kuwa kundi moja na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kitaleta ushindani zaidi baina ya miamba hiyo.
Al Hilal imepangwa Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na timu za Yanga ya Tanzania, TP Mazembe kutoka DR Congo iliyochukua taji la mashindano hayo mara tano na MC Alger ya Algeria.
Timu hizo zitakutana katika mchezo wa kwanza utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ukiwa ni mchezo wa kisasi kwani mabingwa hao wa Tanzania walitolewa na miamba hiyo ya Sudan msimu wa 2022-2023.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema Yanga ni moja ya timu nzuri na bora katika hatua hii na kitendo cha kukutana nayo ni wazi itakuwa mechi ya ushindani, huku akieleza kuna mabadiliko makubwa tofauti na ilivyokuwa mara ya mwisho walipokutana.
“Yanga ya sasa hivi huwezi kuiweka sawa na ile ya mara ya mwisho tuliyocheza nayo, kuna ongezeko la wachezaji bora na wazoefu katika kila eneo, natarajia mchezo baina yetu utakuwa mgumu sana, hivyo jambo kubwa ni maandalizi tu,” alisema Ibenge, Mkongomani aliyewahi kutakiwa na Simba, Yanga kwa nyakati tofauti bila mafanikio.
Ibenge aliongeza kwamba, licha ya kuzisoma vyema timu za hapa Tanzania mara kwa mara anapokuja kuweka kambi, bado haitakuwa ni rahisi kwao, huku akiweka wazi hakuna mchezaji anayepaswa kuchungwa zaidi Yanga kwani wote ni hatari kutokana na aina yao ya uchezaji.
“Siwezi kueleza mchezaji mmoja mmoja ila ninachotambua Yanga imekamilika kila eneo, huwezi kucheza kwa kumuangalia huyu na yule isipokuwa unapambana kuangalia ni jinsi gani utaweza kuwazuia kama timu wasikuletee hatari katika eneo lako la mwisho.”
Katika msimu wa 2022-2023, Yanga na Al Hilal zilikutana katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kusaka tiketi ya kutinga makundi ambapo mechi ya kwanza iliyopigwa Benjamin Mkapa Oktoba 8, 2022 zilitoka sare ya bao 1-1.
Mchezo wa marudiano uliopigwa Oktoba 16, 2022, kwenye Uwanja wa Al-Hilal jijini Omdurman huko Sudan, Yanga ikachapwa bao 1-0, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 na ndipo msimu huo iliangukia Kombe la Shirikisho Afrika na kufika hadi fainali.
Msimu huo ambao Yanga ilifika fainali ilicheza na USM Alger ya Algeria ambapo mechi ya kwanza Dar es Salaam ilipoteza kwa mabao 2-1, Mei 28, 2023, kisha marudiano ikashinda 1-0, Juni 3, 2023 na kukosa ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini.
Yanga imetinga makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo ikiwa na rekodi ya aina yake baada ya kufuzu kwa jumla ya mabao 17-0, kwani katika mechi za raundi ya awali iliiondosha Vital’O kutoka Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.
Hatua ya kwanza Yanga ikaenda kukabiliana na CBE SA ya Ethiopia ambapo mechi yake ya kwanza ikiwa ugenini ilishinda bao 1-0, huku mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar ilishinda mabao 6-0.
Kwa upande wa Al Hilal ambayo ilianzia pia hatua za awali kama Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, michezo yake yote imecheza kwenye nchi mbili tofauti ingawa kwa sasa imeweka kambi Mauritania ambako ndiko inakoshiriki Ligi Kuu.
Al Hilal ambayo inacheza Ligi Kuu ya Mauritania kutokana na changamoto za kiusalama kwao Sudan, hatua ya awali iliiondosha Al Ahly Benghazi ya Libya kwa jumla ya mabao 2-1, kisha raundi ya kwanza ikaitoa San Pedro ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 3-2.
Katika Ligi Kuu Bara Yanga inashika nafasi ya kwanza na pointi zake 24 baada ya kushinda michezo yote minane bila ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Msimu huu kwa ujumla, Yanga imecheza mechi 14 za mashindano tofauti na kushinda zote ikiruhusu bao moja pekee huku ikifunga mabao 34.