Ishu ya straika Simba giza nene, ndugu wafunguka

UNAKWENDA mwezi wa tatu sasa bila ya wapenzi na mashabiki wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini (WPL), kumshuhudia uwanjani aliyekuwa kinara wa mabao msimu uliopita, Aisha Mnunka wa Simba Queens.

Agosti Mosi, mwaka huu, Mwanaspoti iliripoti kuwa nyota huyo wa timu ya taifa (Twiga Stars) ametoroka kambini ikiwa ni siku chache tangu atoke kwenye majukumu ya taifa.

Wakati Simba ikijiandaa na michuano ya kufuzu Klabu Bingwa kwa wanawake iliyoanza Agosti 17 hadi Septemba 4, Mnunka alitoroka kambini bila ya kuomba ruhusa kwa viongozi wa timu hiyo.

Msimu uliopita Mnunka aliibuka kinara wa mabao WPL akifunga 20 katika mechi 18 na kumaliza msimu akiibuka na tuzo tatu za MVP na kikosi bora cha mwaka.

Tangu hapo viongozi wa timu wamekuwa wakifanya jitihada za kumtafuta, lakini hazijafua dafu kwani hata simu anadaiwa kwamba aliizima na hadi leo  hapatikani na hajaripoti kikosini, licha ya Simba kumtaka arejee.

Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu  ambapo kihalali bado ni mchezaji wa Simba Queens.

Ili kujua kwa undani wa sakata hilo, Mwanaspoti iliwatafuta baadhi ya ndugu wa karibu wa Mnunka na marafiki zake na hapa wanaeleza.

Ndugu wa karibu wa mchezaji huyo ambaye hakutaka kutajwa jina alisema aliwaeleza kuwa amepata timu nje ya nchi hivyo wapo kwenye mchakato wa usajili.

“Unajua kama mchezaji huwezi kuuliza sana kwa kuwa ana mtu wa kumsimamia. Pia mimi sijui taratibu za mikataba, lakini alinieleza kuwa amepata timu nje na atakuwa analipwa vizuri,” anasema ndugu wa mchezaji huyo na kuongeza:

“Baadaye nikasikia kwamba haonekani kwenye timu na hata nilipompigia hakuwa anapatikana nikafanya jitihada za kumtafuta nikampata nilipomuuliza kwanini harudi, akasema aliyetaka kumpeleka nje ndie mwenye timu sijui inashiriki ligi hivyo kuna mipango wamepanga na vitu kama hivyo huwezi kuuliza sana wengine hatuna ujuzi navyo,”

Hata hivyo, rafiki wa karibu (jina tunalo) anasema mwenyekiti wa timu inayoshiriki WPL msimu huu alimpa ahadi kwamba atajiunga na timu yake na ikishindikana atamtafutia timu nje.

“Mimi nilikuwepo wakati simu ya huyo kiongozi na baadae nilimuuliza akasema kuna ahadi alimwambia atamtimizia ikiwemo kumnunulia nyumba, usafiri na simu kama atacheza timu yake na atamalizana na Simba kwani bado ana mkataba,” alisema na kuongeza

“Baada ya kunielezea nikamshauri kwanza amalizane na Simba kisha wakimruhusu atakwenda lakini kama unavyojua zile ahadi zilimchanganya na hata anayemsimamia hakuwaza na huwezi amini hadi sasa hakuna ahata kitu kimoja alichotimiza kwenye zile ahadi,” anasema.

Kocha wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka ambaye alimkuza kwenye akademi hiyo, anasema kama angejua anafanya hivyo basi angemshauri mapema.

“Sijawasiliana naye muda mrefu lakini nasikia tu, wanachofanya hawa wasimamizi wao sio sawa, fikiria anakaa nje msimu mzima kama mchezaji lazima ashuke kiwango, lakini hata hao viongozi waliomdanganya hawana nia nzuri na kipaji chake,” anasema Chobanka.

Mratibu wa Simba Queens, Selemani Makanya anasema viongozi wa timu hiyo wamepeleka barua ambayo itasikilizwa hivi karibuni kwa Shirikisho la Soka (TFF) kuhusu utoro wa mchezaji wake Aisha Mnunka .

Makanya anasema wamewaandikia barua TFF kutaarifu juu ya utoro wa mchezaji huyo ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba Queens, ambao ni mabingwa wa Tanzania kwa msimu uliopita.

Anasema Mnunka ni mtoro kazini kwani alitakiwa kuripoti Simba mara baada ya majukumu ya timu ya taifa, lakini hakufanya hivyo na hakuna mawasiliano yoyote hadi sasa ambapo Ligi tayari imeanza.

Makanya anasisitiza kuwa nyota huyo hakutoa taarifa yoyote kuhusu utoro na uongozi umefanya jitihada zote za kumtafuta bila mafanikio na hata katika simu hapatikani kwa kuwa amebadilisha namba.

“Aisha Mnunka bado ni mchezaji wa Simba, ana mkataba wa mwaka mzima, lakini hatuna taarifa rasmi, baada ya kurejea kikosi cha timu ya taifa alitakiwa kuripoti kambini lakini hakuripoti na hakuna taarifa yoyote aliyotoa kwa viongozi kama anaumwa au la hivyo tumepeleka malalamiko TFF,” anasema Makanya

“Kama mnavyojua kila kitu kinakwenda na sheria na taratibu naTFF wao ndio wasimamizi hivyo tunasubiri hukumu ambayo itasikilizwa hivi karibuni.”

Kanuni za TFF za mwaka 2023/24 sura ya 14 kifungu cha usajili kinaeleza kuwa mchezaji ana ana uhuru wa kujisajili klabu nyingine iwapo kutakuwa na maelewano ya klabu na timu inayotaka kumsajili.

“Mchezaji ana uhuru wa kujisajili na klabu nyingine katika msimu mmoja iwapo kutakuwa na maelewano kati ya klabu yake na kile kinachotaka kumsajili au atakuwa amemaliza mkataba na klabu yake,” inasema kanuni

“Ukiukaji wowote wa masharti ya usajili ambao haujaanishwa ipasavyo kwenye kanuni hizi bado utastahili vikwazo vinavyofaa au kutozwa kwa faini kati ya shilingi laki tano (500,000/-) na shilingi milioni tano (5,000,000/-), au zuio la kucheza kwa mchezaji. Mpaka Masharti ya msingi kiutaratibu yawe

yametimizwa au na adhabu ya faini/kufungiwa kwa muhusika yoyote endapo kuna makosa binafsi ya kiutendaji na fidia kwa athari zilizosababishwa na ukiukwaji au/na mapungufu hayo makubwa ya taratibu za usajili yaliyo na athari.”

Related Posts