Dar es Salaam. Vigogo wawili wa chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP), waliofungua kesi mahakamani kutaka vigogo wengine wawili wa chama hicho waachie ngazi kwa kukiuka katiba ya UPDP, wamekwaa kisiki kortini.
Moja ya hoja iliyokuwa ikilalamikiwa ni hatua ya wajibu maombi kumteua Twalib Kadege, kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2020 kinyume na Katiba ya UPDP kuhusiana na uteuzi huo.
Vigogo hao, Mbwana Kibanda ambaye ni Mweka Hazina na Ramadhan Abdallah ambaye ni Naibu Mweka Hazina, walifungua maombi namba 128 ya 2022 dhidi ya Abdalah Khamis ambaye ni Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu, Hamad Ibrahim.
Hata hivyo, maombi hayo yalikutana na kisiki kortini, baada ya wajibu maombi kuwasilisha pingamizi kupinga maombi hayo wakidai yana dosari kisheria kwani iliyostahili kushitakiwa ni Bodi ya Wadhamini ya chama hicho na sio viongozi.
Pingamizi hilo limekubaliwa na Jaji David Ngunyale wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam kupitia uamuzi wake alioutoa Oktoba 29, 2024 baada ya kusema sababu za pingamizi lililowekwa zina mashiko hivyo anaitupa kesi hiyo.
Katika maombi yao, vigogo hao wawili walidai kuwa wajibu maombi walikuwa wamekiuka vifungu vya Katiba ya UPDP kwa kuitisha kikao cha Kamati Kuu ya UPDP Desemba 01, 2019 bila kufuata miongozo ya Katiba ya chama hicho.
Mbali na hoja hiyo, walidai viongozi wenzao walikiuka Katiba kwa kumruhusu Twalib Kadege kuhudhuria kikao wakati si mjumbe na waliwafukuza wajumbe wa Kamati Kuu na mkutano mkuu wa UPDP pasipo kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.
Halikadhalika walikuwa wanadai kuwa wajibu maombi hao waliitisha mkutano mkuu Julai 20, 2020 na kuhudhuriwa na wajumbe ambao sio halali na pia kumteua Twalibu Kadege kuwa mgombea urais wa UPDP uchaguzi mkuu 2020.
Hivyo wakaiomba mahakama itamke kuwa, wajibu maombi walikiuka katiba ya UPDP na wanatakiwa kuachia ngazi na pili, iwaamuru kuitisha vikao vya Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na mkutano mkuu wa UPDP.
Pingamizi la wajibu maombi
Hata hivyo, wajibu maombi katika kesi hiyo waliwasilisha pingamizi lenye hoja mbili kwamba maombi hayo yalikuwa na dosari kwa kutoiunganisha Bodi ya Wadhamini ya UPDP na pili, waombaji walishitaki watu wasiostahili.
Akijenga hoja kuhusu pingamizi hilo, wakili Desidery Ndibalema aliyewawakilisha wajibu maombi, alisema wateja wake ni viongozi tu wa kawaida wa UPDP na malalamiko ya waleta maombi ni maamuzi ambayo hakuyafanya kwa vyeo vyao.
Badala yake, alisema maamuzi hayo yalifanywa kwa mujibu wa Katiba ya UPDP, maamuzi ambayo yalipata baraka za Msajili wa vyama vya siasa nchini kama sheria ya Vyama vya Siasa Nchini inavyoelekeza.
“Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kupinga maamuzi hayo ni lazima awaunganishe bodi ya wadhamini ya UPDP ambayo inaundwa kwa mujibu wa kifungu 21(1) cha sheria ya vyama vya siasa nchini. Bodi ndio ilikuwa sahihi kushitakiwa,”alisema.
Katika hoja ya pili, wakili Ndibalema alisema wajibu maombi hawawezi kushitakiwa kama viongozi waandamizi wa UPDP kwa sababu chochote wanachokifanya, wanafanya kwa mujibu wa katiba au maagizo ya vikao.
“Maamuzi hayo ya vikao juwa baadae yanapata baraka za Msajili wa vyama vya siasa kwa hiyo kuyapinga hakuwezi kuelekezwa kwa baadhi ya viongozi wa UPDP bali ni lazima yawe dhidi ya chama,” alisisitiza wakili huyo katika hoja yake.
Akijibu hoja za wajibu maombi, wakili Dominicus Nkwera aliyewawakilisha waleta maombi alisema wajibu maombi walishitakiwa kwa vile ni viongozi wa UPDP wakiwa ni Makamu Mwenyekiti wa UPDP na Katibu Mkuu wa chama hicho.
“Waombaji hawawezi kuishitaki Bodi ya Wadhamini ya UPDP kwa sababu haipo baada ya muda wao wa uongozi kumalizika na kwamba wajumbe wa bodi walisajili kwa miaka mitano na muda ulipoisha haukuhuishwa,” alisema.
Mbali na hoja hiyo, wakili alisema wajumbe watatu walishafariki na kuongeza kuwa Katiba ya UPDP iko kimya kuhusu ni nani wa kushitakiwa kwa niaba ya chama hivyo kwa vile wajibu maombi ni wanachama hai walichagua kuwashitaki.
Wakili Nkwera alisisitiza ni wajibu wa mahakama kumuunganisha yeyote inayoona anafaa na kwamba hoja ya kuiunganisha bodi ya wadhamini imeletwa kabla ya muda na inahitaji ushahihidi kwa vile ni hoja ya kisheria.
Katika uamuzi wake, Jaji Nyunyale alisema baada ya kuzipitia hoja za pingamizi, ameridhika ni hoja za kisheria hivyo wajibu wa mahakama ni kuamua kama zina mashiko ama sivyo katika kuamua, atazitolea maamuzi hoja mbili pamoja.
Jaji alisema kutokana na maombi yaliyowasilishwa na waleta maombi, hakuna shaka kuwa hoja kuu ya maombi inatokana na mkutano wa UPDP uliofanyika Desemba 1,2019 na Julai 20,2020 ambao wajibu maombi pia walikuwa wajumbe.
Kulingana na Jaji, kwa kuwa UPDP ni chama cha siasa kilichosajiliwa, sheria inataka mara baada ya kusajiliwa ni lazima kiteue wajumbe wa Bodi ya Wadhamini kwa ajili ya kusimamia mali za chama, shughuli za chama na uwekezaji wa chama.
“Hakuna ubishi kuwa kuna wakati UPDP ilisajili Bodi yake ya wadhamini. Lakini Nkwera (wakili) ana maoni kuwa muda wa bodi hiyo ulishaisha kwa maelezo kuwa miaka mitano ilishamalizika tangu ilipoteuliwa kwa mujibu wa Katiba,”alisema Jaji.
“Lakini akasema miongoni mwa wajumbe wa bodi wapo ambao walishafariki na nafasi zao hazikujazwa hivyo asingeweza kuishitaki bodi ya wadhamini,”alieleza Jaji akirejea hoja ya wakili wa waleta maombi hayo.
Jaji alisema kwa maoni yake, wasilisho la wakili huyo ni hoja zilizotoka kwa wakili ambazo hawezi kuvutiwa kuzishughulikia kwa vile hazionekani popote katika hoja zao zilizomo katika maombi yao na akatoa mifano ya misimamo ya kisheria.
“Swali linalofuata ni kama waleta maombi walikuwa sahihi kuwashitaki wajibu maombi. Katika hili nakubaliana na wakili Ndibalema kwamba waleta maombi walipaswa kuishitaki Bodi ya wadhamini ya UPDP na sio wajibu maombi,”alisema.
“Hii ni kwa sababu kila kilichofanywa katika mkutano kilikuwa ni kwa niaba ya UPDP ambayo ni taasisi. Kwa msingi huo, ninaridhika kuwa kile ambacho waombaji wanakilalamikia, watu sahihi wa kuwashitaki ni Bodi ya wadhamini”
Jaji alisema haikuwa sahihi kuwashitaki viongozi hao kwa vile maamuzi hayakuwa yao binafsi bali yalikuwa ni maamuzi ya chama kama taasisi na madhara ya kumshitaki mtu asiyestahili, ni maombi hayo kutupiliwa mbali hivyo akayatupa.