LICHA ya Pamba Jiji kushindwa kukusanya pointi za kutosha katika mechi kumi ilizocheza hadi sasa katika Ligi Kuu, kocha wa Pamba Jiji, Fred Felix ‘Minziro’ amesema kuna mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hicho akiamini muda mfupi ujao kila kitu kitabadilika na watu kusahau machungu.
Minziro ameiongoza Pamba Jiji kwenye mechi mbili kati ya kumi zilizochezwa na zote ikipoteza kwa kufunga bao 1-0 na Tabora United na Namungo mtawalia, lakini kocha huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, Geita Gold na Kagera Sugar aliyetambulishwa Oktoba 17, akichukua nafasi ya Goran Kopunovic ameliambia Mwanaspoti, wachezaji wa timu hiyo wameanza kuingia katika mfumo.
“Hatujapata matokeo lakini kwa namna moja ama nyingine kuwa mabadiliko makubwa kutokana na wachezaji kuanza kuingia kwenye mfumo na kutoa ushindani kwa timu pinzani.”
“Nimejaribu kutoa nafasi kwa kila mchezaji ili waonyeshe uwezo na vipaji walivyonavyo lengo ni kuona ni mchezaji gani ambaye anaweza kuwa msaada kutokana na timu kukosa matokeo kwa muda.”
Anaamini bado wana nafasi ya kufanya vizuri kwa kuhakikisha wanaipambania timu hiyo iweze kucheza tena ligi msimu ujao huku akikiri kuwa sio kazi rahisi lakini lolote linaweza kutokea.
Alisema ligi ni ngumu mipango imara na wachezaji kujitolea kwa kuipambania Pamba Jiji ndio njia sahihi ambayo itawatoa nafasi waliyopo na kusonga mbele huku akisisitiza kuwa morali nzuri itarejea mara baada ya kupata pointi kitu ambacho ndio anapambania.
Timu hiyo iliyorejea katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuisotea kwa miaka 23 tangu iliposhuka 2001, inashika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa ndio timu pekee ambayo haijaonja ushindi, kwani imetoka sare tano na kupoteza nyingine tano katika michezo 10 iliyocheza hadi sasa na mechi ijayo.