Mauaji ya waandishi duniani yaongezeka kwa asilimia 38 – DW – 02.11.2024

Ripoti hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Utamaduni UNESCO inaonyesha kuwa waandishi 162 waliuwawa wakiwa kazini hiyo ikiwa ongezeka la asilimia 38.

UNESCO kupitia kwa mkurugenzi wake mkuu Audrey Azoulay inasema ongezeko hilo la mauaji linatia hofu kwani hakuna hatua iliyochukuliwa katika karibu visa vyote hivyo vya mauaji.

Mataifa yawajibike na kuwachukulia hatua wahusika

Azoulay ameyataka mataifa duniani kuongeza juhudi kuhakikisha kwamba wanaotenda vitendo hivyo vya kihalifu vya kuwauwa waandishi wanachukuliwa hatua.

Mshukiwa wa mauaji ya mhariri mmoja nchini Uturuki akikamatwa na polisi
Mshukiwa wa mauaji ya mhariri mmoja nchini Uturuki akikamatwa na polisiPicha: MUSTAFA OZER/AFP via Getty Images

Katika kipindi cha miaka miwili hiyo, kanda ya Amerika Kusini na visiwa vya Caribbean ndizo zilizoshuhudia mauaji mengi ya waandishi, 61 wakipoteza maisha.

Kulingana na UNESCO maeneo ambayo hayana hatari kubwa kwa waandishi ni Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi ambapo waandishi 6 pekeyake ndio waliouwawa katika kipindi hicho cha miaka miwili.

Ripoti hiyo pia imepata kuwa idadi kubwa ya waandishi waliuwawa katika maeneo yenye mizozo mwaka 2023, waandishi 44 wakiwa walipoteza maisha, hiyo ikiwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017 ambapo idadi ya waandishi waliokuwa wanafariki katika maeneo kama hayo ilikuwa inapungua.

Baadhi ya nchi kutotoa ushirikiano na UNESCO

Kati ya waandishi waliouwawa mwaka 2022 na 2023, 14 walikuwa wanawake na watano kati yao walikuwa kati ya umri wa miaka 15 hadi 24.

Kamera ya mwandishi aliyejeruhiwa na bomu katika vita vya Mashariki ya Kati
Kamera ya mwandishi aliyejeruhiwa na bomu katika vita vya Mashariki ya KatiPicha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Kati ya nchi 75 ambazo UNESCO iliwasiliana nazo kwa ajili ya kupata idadi za waandishi waliouwawa, 17 hazikutoa majibu kabisa na nchi 9 zilikubali ombi hilo ila hazikutoa jawabu.

Kila mwaka UNESCO hufanya kampeni ya kuuhamasisha umma dhidi ya unyama wa kuuwawa kwa waandishi wa habari.

Mwaka huu shirika hilo la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano kuhusiana na usalama wa waandishi wakati wa kuripoti kuhusiana na mizozo. Mkutano huo utafanyika katika Mji Mkuu wa Ethiopia Addis Ababa mnamo Novemba 6.

Related Posts