MIRADI YA TACTIC KUIMARISHA MAZINGIRA YA UFANYAJI WA BIASHARA NCHINI- MHE. KATIMBA.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawaka za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Zainabu Katimba amesema kukamilika kwa Miradi ya TACTIC mkoani Kigoma kunatarajiwa kuleta tija kubwa kwa uchumi wa Mkoa huo pamoja na kukuza mazingira bora ya ufanyaji wa biashara kote Tanzania.

Mhe. Katimba ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 02, 2024 wakati akihutubia wananchi kwenye Viwanja vya Mwanga Center Kigoma Ujiji wakati wa hafla ya utiaji saini ujenzi wa soko kuu la Mwanga na Soko la samaki Katonga katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa TACTIC unaosimamia na wizara ya TAMISEMI, kando ya miradi mingine yenye thamani ya zaidi ya Trilioni 2.9 za Kitanzania sawa na Dola za Marekani Bilioni 1.108.

Mhe. Katiba aliyemuwakilisha waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema miradi hiyo pia inatarajiwa kupandisha pato la Halmashauri za Mkoa huo kutokana na maboresho makubwa na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya usafiri na usafirishaji, vizimba vya biashara, maduka pamoja na huduma nyingine za kijamii zitakazotekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 12 ya utekelezaji wa mradi huo.

Katika hatua nyingine Mhe. Katimba amehimiza suala la uwajibikaji kwa kila anayehusika na utekelezaji wa ujenzi wa Masoko hayo, akitaka ikamilike kwa wakati na kwa ubora ili tija yake ionekane mapema kwa wananchi.

Aidha pia amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Novemba 27, 2024 ili kuchagua Viongozi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha kuwa wanapatikana Viongozi bora watakaoweza kusimamia ujenzi na uendeshaji wa miradi ya TACTIC inayotekelezwa kwenye Halmashauri za Miji, Majiji na Manispaa zaidi ya 40 za Tanzania bara.





Related Posts