Jumla ya Shilingi Bilioni 16 na Milioni 495 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi na Maboresho makubwa ya Masoko ya Kimkakati Kata ya Mwanga na Soko la samaki Katonga, yaliyopo Kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa TACTIC unaofadhiliwa na Benki ya dunia.
Mradi wa TACTIC wenye thamani ya takribani dola za Marekani Milioni 410 ukifadhiliwa na Benki ya dunia, unalenga kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania pamoja na kuzijengea uwezo Halmashauri za Tanzania bara ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi na uendelezaji miji, Majiji na Manispaa pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Akiwa Mjini Kigoma wakati wa utoaji wa taarifa ya ujenzi wa masoko hayo mawili kwaniaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara Vijjjini na Mijini TARURA leo Jumamosi Novemba 02, 2024, Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema ujenzi wa masoko hayo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi kumi na mbili na kwasasa tayari Mkandarasi ameshapatikana.
Mhandisi Kanyenye amesema katika soko la Mwanga jumla ya wafanyabiashara 4140 watanufaika na ujenzi huo kutokana na maboresho makubwa ya ujenzi wa vizimba 1000, maduka 3040 pamoja na migahawa takribani 100 kwaajili ya mamalishe na babalishe wa Mkoa wa Kigoma suala litakaloongeza makusanyo kwa Halmashauri kutoka Shilingi Milioni 450 kwa mwaka hadi kufikia Bilioni 1.400.
Aidha kukamilika kwa soko la Samaki Katonga kunatarajiwa kunufaisha wafanyabiashara zaidi ya 2000 kutoka wafanyabiashara 270 wa awali ambapo jumla ya Vizimba vipya 300 vitajengwa, fremu 800, vyumba baridi (Cold room)10, ujenzi wa eneo la kukaushia samaki pamoja na maegesho ya magari na Pikipiki na hivyo kuongeza makusanyo ya mapato ya Halmashauri kutoka Milioni 31.125 kwa mwaka hadi kufikia zaidi ya Milioni 183.240 kwa mwaka.