Mukwala: Nimewasikia! | Mwanaspoti

STEVEN Mukwala amefunga bao la pili katika Ligi Kuu Bara wakati akiipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, kisha kuitoa msimamo wake akisema amefurahishwa na jinsi mashabiki na benchi la ufundi kiujumla walivyompongeza, lakini amesisitiza anaamini ataendelea kuwapa raha kadri atakapopata nafasi.

Mukwala alifunga bao dakika za jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma na kuifanya Simba ichupe kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo ikifikisha pointi 22 ikilinganana na Singida Black Stars yenye alama kama hizo, lakini zikitofautiana kwa mabao ya kufungwa na kufungwa.

Hilo lilikuwa bao la pili kwa straika huyo aliyesajiliwa msimu huu kutoka Asante Kotoko ya Ghana kwani la kwanza alilifungwa wakati Simba ikiishindilia Fountain Gate kwa mabao 4-1 katika mechi iliyopigwa Agosti 25 na akizungumza na Mwanaspoti mapema jana, nyota huyo alisema amefurahia kuipa timu hiyo ushindi.

Mukwala alisema bao hilo limemuongezea hali ya kujiamini baada ya kuwa na ukame wa muda mrefu wa kufunga mabao na kusisitiza atahakikisha anaendelea kuipambania timu hiyo kila anapopata nafasi kikosini.

“Furaha yangu haielezeki kwa siku ya jana (juzi), ilikuwa ni mechi ngumu na yenye ushindani niwashukuru wenzangu kwa moyo wa kujituma hadi mwisho bila ya kukata tamaa, hii ni motisha kwetu ya kuendelea kupambana zaidi kwa kila mchezo,” alisema Mukwara na kusisitiza amewasikilia wote waliokuwa nyuma yake.

Straika huyo, aliongeza kuwa kusema ushindani uliopo unaongeza ari ya kila mmoja wao kupambana akipewa nafasi ya kucheza, hivyo licha ya hivi karibuni kutocheza kikosi cha kwanza mara kwa mara ila hana hofu kwa sababu ni moja ya njia ya kufikia malengo yao.

“Nitafanya kilichokuwa bora kwa manufaa ya timu kwa ujumla, naheshimu kila mmoja wetu anayecheza kwa sababu tupo malengo yaliyokuwa sambamba, kikubwa kwangu ni kupambana nikipata nafasi ili kwa pamoja tutimize na kufikia inachokitaka klabu,” alisema.

Nyota huyo ametua Simba huku akikumbukwa zaidi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 14 akiwa na kikosi cha Asante Kotoko ya Ghana nyuma ya kinara mshambuliaji wa Berekum Chelsea, Stephen Amankonah aliyefunga mabao 16, akiichezea timu hiyo.

Pia aliibuka mchezaji bora wa Ligi ya Ghana Desemba mwaka jana akiwa na kikosi hicho cha Asante Kotoko aliyojiunga nayo Agosti 2022 akitokea Klabu ya URA ya kwao Uganda na katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na kutoa asisti tano.

Akiwa URA, Mukwala alicheza kwa misimu mitatu kuanzia mwaka 2020 ambapo msimu wa kwanza 2019/2020 aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda akifunga mabao 13 na msimu wa 2020/2021, akafunga 14 kisha 2021/2022 akatupia tena kambani mabao 13.

Ushindi huo ni wa saba wa Ligi Kuu Bara kwa Kocha Mkuu, Fadlu Davids tangu atambulishwe ndani ya kikosi hicho Julai 5, mwaka huu akichukua nafasi ya Abdelhak Benchikha aliyeondoka Aprili 28, mwaka huu na kutua JS Kabylie ya kwao Algeria.

Fadlu amejiunga na Simba ikiwa ni muda mfupi tangu aipe ubingwa wa Ligi Kuu Morocco, Raja Casablanca akiwa msaidizi wa Kocha Mkuu, Josef Zinnbauer raia wa Ujerumani ambaye kwa sasa pia ameondoka na kujiunga na Al Wehda FC ya Saudi Arabia.

Kiujumla Fadlu ameiongoza Simba katika michezo tisa ya Ligi Kuu Bara msimu huu, akishinda saba, sare mmoja na kupoteza pia mmoja na kukusanya pointi 22, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 17 na kuruhusu matatu tu.

Related Posts