Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ameadhimisha miaka minne ya utawala wake akiahidi kuendelea kuwaleta vijana karibu katika masuala yote ya kitaifa, huku akichukua hatua za kutatua changamoto zinazowakabili.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya miaka minne ya utawala wake kwenye uwanja wa Gombani, Pemba, leo Novemba 2, 2024, Dk Mwinyi amesisitiza kuwa vijana ndio nguvu na uhai wa Taifa.
Sherehe hizo, zilizoandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), zimehusisha uzinduzi wa kampeni ya “Kijana na Kijani” na kuwahamasisha vijana hao kushiriki katika ujenzi wa nchi na kuleta maendeleo kwa uzalendo.
Dk Mwinyi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, amezipongeza jumuiya zote za chama hicho kwa kazi zinazozifanya.
“Ahadi yangu kwa vijana na uongozi wa UVCCM na vijana wote ni kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika mambo yote na kuwashirikisha katika mambo yote muhimu yanayohusu Taifa letu,” amesema.
“Vijana ndio uhai na nguvu kazi ya Taifa letu na siku zote huwa wanabeba ndoto iliyobora zaidi, kwa mnasaba huo lazima Serikali zinazoongozwa na CCM zifanye kazi kwa karibu na jumuiya ya vijana kwa ajili ya kuzifanyia kazi changamoto zote zinazowakabili vijana wetu,” ameongeza.
Dk Mwinyi aliapishwa kushika wadhifa wa Urais, Novemba 2, 2020 na aliyekuwa Jaji Mkuu wakati huo, Othman Omar Makungu baada ya kushinda kiti hicho kwa asilimia 76.27 ya kura dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, aliyepata asilimia 19.87.
Rais Mwinyi amesema chama hicho kina mfumo mzuri wa kuwandaa vijana katika siasa, uongozi na uzalendo kupitia jumuiya ya vijana.
Hivyo, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha UVCCM kuwahimiza vijana wajiunge na jumuiya hiyo kwa umoja na ari ya kufanya kazi kwa kujituma na kushiriki katika kazi za maendeleo kwa kuwa nchi itajengwa na vijana.
“Kwa kuwa vijana ndio wenye nguvu zaidi na wana kasi zaidi ya kufanya shughuli za kujenga nchi yetu kwa kujitolea, miongoni mwa mambo ya msingi ambayo Serikalii inayazingatia ni washirikisha katika uongozi na vyombo vya kutoa maamuzi,” amesema.
Dk Mwinyi amesema: “Nyote ni mashahidi namna Serikali inavyozingatia vijana katika teuzi mbalimbali na kuhakikisha wanapata fursa ya kuwakilisha katika vyombo vya maamuzi kama Bunge na Baraza la wawakilishi.”
Amesema Serikali imeanzisha mabaraza ya vijana kuanzia ngazi ya shehia hadi Taifa ili yawe majukwaa muhimu ya vijana kuzungumzia changamoto zao na kuzipeleka katika vyombo vinavyohusika.
Amesema kwa kuzingatia umuhimu wa elimu, Serikali imewekeza nguvu kubwa katika sekta hiyo kuhakikisha vijana wanaandaliwa kupata nguvu kazi yenye taaluma na uzalendo.
Kwa upande wa elimu ya juu, amesema Serikali imeongeza fedha kwa bodi ya elimu ya juu kutoka Sh11 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh33 bilioni mwaka huu.
Amesema wameimarisha mafunzo ya amali kwa vijana wanaokosa fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari, vimejengwa vyuo vitano ili wapate elimu ya ufundi kuwawezesha kujiajiri na kuajiriwa katika sekta binafsi.
Jambo lingine amesema Serikali inaongeza jitihada za uwekezaji na fursa za ajira, hususani kwa vjana ambao katika kipindi cha miaka minne miradi 330 yenye mtaji wa Dola za Marekani 5.4 bilioni sawa na zaidi ya Sh11 trilioni imesajiliwa na inatarajiwa kuzalisha ajira 18,000 katika sekta za utalii, viwanda na majengo.
Pia amesema inaendelea kuifungua Pemba kwa kuendeleza kazi ya ujenzi wa mindombinu ya barabara za mjini na vijijini, kuzifanyia matengezo bandari za Mkoani na Shumba, na kuanza matayarisho ya uwanja wa ndege na kuimarisha eneo la uwekezaji la Micheweni ambako wawekezaji wengi wameanza kuonyesha nia ya kuwekeza.
Amewataka vijana kuwa wamoja, wapenda amani na wazalendo; wajiepushe na mambo ambayo yanaweza kuwaharibia maisha yao, huku wakizitumia fursa zilizopo kujiendeleza kitaaluma na kiuchumi.
Hata hivyo, Dk Mwinyi amesema bado kuna taarifa kwamba vijana wengi hawajajiandikisha katika daftari la mpigakura licha ya kufikisha umri, hivyo waelimishwe na kuhamasishwa kujiandikisha.
Katika sherehe za kilele, Dk Mwinyi alipokea kadi 1,135 za waliodaiwa walikuwa wanachama wa ACT- Wazalendo wanaojiunga na CCM.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao, Raya Raya amesema yeye na wenzake wameona CCM kuna ukweli na wanayoahidi wanatenda, hivyo hakuna budi kuondoka upande waliokuwa.
“Nimezunguka vijiji vyote Tanzania na vijiji vyote Zanzibar tuungane pamoja wenzangu kujiunga na CCM. Hili ni kundi dogo nimekuja nalo. kuna kundi lingine lipo nyuma yangu nalo linatarajia kujiunga,” amesema.
Naye Abbas Ali Khamis, kiongozi wa kundi la wanaodaiwa walikuwa wanachama wa ACT-Wazalendo Mtambwe amesema wameanguka wakanyanyuliwa, hivyo wameamua kujiunga na CCM kuendeleza mapambano.
“Tunashukuru mmetupokea tupo pamoja kwa ajili ya kuiendeleza Zanzibar,” amesema.
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Jokate Mwegelo amesema vijana watahakikisha Dk Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan wanashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu mwaka 2025.
“Umezima chokochoko, umezima wote waliosema hautaweza, umezima uzandiki na ukawasha taa ya amani, upendo na maendeleo. Tunakuahidi ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” amesema.
Jokate amesema Watanzania wana imani na viongozi hao na kwamba: “Tunakwenda nao mwaka 2025 hadi 2030, tumejipanga vya kutosha kuhakikisha tunawafunga magoli ya haki kwa madiwani, wabunge na urais.”
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Ali Kawaida amesema Dk Mwinyi amekuwa na dhamira ya dhati kuhakikisha anawaletea wananchi maendeleo, hivyo vijana wapo nyuma yake kuhakikisha dhamira hiyo inatimia.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Muhamed Dimwa amesema CCM inaridhishwa na utekelezaji wa ilani ya chama, hivyo haina shaka kwamba Dk Mwinyi ameivusha kwa miaka minne kwa kuwa tayari ilani imeshatekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100 na ataweza kuivusha kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.
“CCM hakina shaka ameweza kuongoza kwa umahiri ataweza kukivusha chama kwa kipindi kingine,” amesema.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Hemed Suleman Abdulla amesema wanampongeza Dk Mwinyi kwa kuitendea haki nafasi yake ya makamu mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Zanzibar.
Amesema Pemba waliokuwa wanaijua zamani si ya sasa, akieleza wana-Pemba wanafahamu thamani ya maendeleo na wanafahamu kazi inayofanywa na Dk Mwinyi.
“Tutafanya kazi, wananchi wa Pemba siasa ni maendeleo na siasa si ugomvi. Dk Mwinyi ndio mtu sahihi wa kumpa miaka mitano mingine kuliongoza Taifa hili, hatuna mbadala wa Dk Mwinyi, hatuna mbadala wa CCM,” amesema Abdulla ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Matar Zahor amesema wananchi wa mikoa miwili ya Pemba wana mengi ya kujivunia ambayo yamefanywa katika kisiwa hicho.
“Amejenga madarasa zaidi ya 61 katika mikoa miwili, na shule za ghorofa 13 na kupata ajira zaidi ya 1,500 na sasa kuna vibali kwa ajira 600 kwa walimu,” amesema.
Amesema: “Vyoo 953 vimejengwa kwenye shule na kuimarisha Hospitali ya Abdallah Mzee kwa kupata vifaa vya kisasa na ujenzi wa vituo vya afya vinane.”
Amesema wazee 12,537 wanapata pensheni jamii ya Sh50,000 kila mwezi. Pia, Pemba wamepata Sh14.5 bilioni kwa ajili ya kuwaunganishia umeme wananchi kati ya hizo Serikali imechangia Sh10 bilioni.