Dar es Salaam. Ikiwa ni siku moja tangu taarifa ya kutoweka kwa Mkurugenzi wa Dar24 Media, Maclean Mwaijonga zisambae katika mitandao ya kijamii, Jeshi la polisi limesema limeanza uchunguzi.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Novemba 2, 2024 na mmoja wa viongozi wa Datavision International Ltd, William Kihula kupitia mitandaoni, imesema, Mwaijonga ambaye pia ni mtendaji wa kampuni hiyo, hana kawaida ya kutorudi nyumbani lakini mpaka sasa hapatikani.
“Wakati akitoka ofisini alikuwa na gari aina ya Toyota Prado nyeusi yenye namba za usajili T 645 DEE.
“Tunaomba msaada wa vyombo vinavyohusika na wanahabari kwa pamoja zitusaidie kupaza sauti ili kumpata kiongozi wetu na utakapomuona yeye au gari yake tupe taarifa kwa namba hii,” amesema.
Amedai kuwa tangu wametoa taarifa hiyo Polisi, bado hawajajibiwa.
“Tangu tumetoa taarifa hilo hatujapata mrejesho wowote, kwa sababu saa 24 zimepita tumesharipoti tukio hili polisi kituo cha Osterbay,” amedai.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi leo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wamepata taarifa hiyo na wameanza uchunguzi.
“Hiyo ni taarifa na mimi nimeiona kwa hiyo na mimi nafuatilia. Ndugu walikuja wakatuambia nini na nini, lakini tukimwangalia sisi hatuna rekodi naye za criminality (jinai), kwa hiyo na sisi tunafuatilia,” amesema Muliro.