Rajabu: Mwenyekiti CCM Tanga anayefuata nyayo za Mkapa

“Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (marehemu) ndiye alinivutia na kuona iko siku ninaweza kuwa mwanasiasa mkubwa hapa Tanzania,” hayo ni maneno ya Rajabu Abdallahman Mwichande, mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga

Rajabu alishinda nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa ndani ya chama uliofanyika mwaka 2022 na wako wana CCM ndani ya mkoa wa Tanga na nje ya mkoa huo wanaofuatilia mafanikio ya kiongozi huyo na kumtabiria kufika mbali.

Hii ndio imemtokea Rajabu, mkazi wa Kijiji cha Mwera Wilaya ya Pangani, aliyezaliwa Februari 5, 1977 akiwa baba wa watoto saba na wake wawili.

Mwananchi ilimtafuta na kufanya mahojiano na kada huyu wa CCM ambaye alionekana kuwa na ushawishi wa kisiasa kwa eneo hilo, kufahamu zaidi historia na jinsi gani ameingia kwenye mambo ya siasa hadi alipofikia sasa.

Anaeleza kuwa mwanasiasa ambaye alimvutia kwa mara ya kwanza na kutamani siku moja awe mwanasiasa mkubwa, ni Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya tatu, aliyemuona kwenye kampeni za kugombea urais wilayani Pangani mwaka 1995.

Anaeleza kuwa siku hiyo ya mkutano, yeye alikuwa ndio anatoka kufanya mtihani wake wa mwisho wa kumaliza elimu ya msingi eneo la Pangani Magharibi na wakati wanatoka msafara wa mgombea ulikuwa unawasili kwenye uwanja wa mkutano.

Siku hiyo, Mkapa alifika Wilaya ya Pangani katika kampeni na alikuwa akinadiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mzee Ngulamali na kikubwa kwake kilichomvutia ni jinsi alivyokuwa akiahidi jinsi gani atakwenda kutatua kero za wananchi.

“Mwaka 1995 wakati tunaingia kwenye uchaguzi wa kwanza kwa mfumo wa vyama vingi, ndio mwaka ambao nilikuwa ninamaliza darasa la saba,” anasema Rajabu.

“Ndio siku ambayo mgombea wa urais wa CCM hayati Benjamin William Mkapa ndio alikuwa amekuja Pangani kufanya kampeni zake za urais, akiwa ameongozana Mzee Jakaya Kikwete, Ngulamali na viongozi wengine maarufu,” anasema.

Msafara huo ndio uliomvutia na kujiwekea ahadi kwamba ataingia tu kwenye siasa.

Anasema watu wengi ambao aliwaona siku hiyo alikuwa akiwasikia tu ila siku hiyo wote aliwaona kwa sababu ya matukio yaliyokuwa yakitokea uwanjani hapo yalimpa shauku na motisha zaidi kuyafuatilia.

Baada ya kwenda sekondari akitoka shule alipenda kuwa karibu na wanasiasa wakubwa wa Wilaya ya Pangani akiendelea kujifunza namna wanavyofanya kazi zao, na nini wanafanya kwenye jamii inayowazunguka kupitia siasa zao.

Anaeleza kuwa nafasi ya kwanza kuipata kama mwanasiasa aligombea na kupata nafasi ya balozi wa shina, huku akiendelea na masomo ya dini katika madrasa za Wilaya ya Pangani baada ya elimu ya sekondari.

Na akiwa balozi alipewa nafasi ya kuwa mjumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Tanga na baadaye akashika tena nafasi ya mjumbe wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Pangani na vyinginezo.

Mwaka 2014 aligombea nafasi ya mwenyekiti wa Kijiji cha Pangani Magharibi na kushinda kwa zaidi ya kura 300 dhidi ya kura 18 za anayemfuatia, ikiwa ni mwendelezo wa safari yake ya kisiasa.

Ilipofika wakati wa uchaguzi mwaka 2017, alitaka kugombea nafasi ya mwenyekiti wa CCM wilaya lakini kutokana na kanuni kuzuia mwenye nafasi nyingine kugombea alikwama kuingia kwenye kinyang’anyiro huku akiwa mwenyekiti wa kijiji.

Rajabu anasema mwaka 2019 wakati anamalizia muda wa uenyekiti wa kijiji alifuatwa na Jumaa Aweso, waziri wa Maji wa sasa akiwa na jopo la wazee na kumtaka kugombea nafasi ya mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Pangani na aliposhiriki uchaguzi huo alishinda nafasi hiyo.

Anasema baada ya kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi huo, Chama cha Wananchi (CUF) kilikuwa kimeshika maeneo mengi ya wilaya hiyo, hivyo jambo la kwanza lilikuwa ni kuifuta kichwani kwa wananchi na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Nikaanza ziara katika kata 14 za Pangani kusikiliza na kutatua kero za wananchi kichama na Serikali na kila kata nililala siku mbili na nilikuwa nikilala kwa balozi wa eneo husika kwa siku zote 28. Wakati huo upinzani Wilaya ya Pangani ulikuwa moto sana, maana ilikuwa ni asilimia 50 kwa 50 kwa hiyo ilikuwa ni moto kweli kweli”.

Anaeleza kuwa wananchi walianza kumwelewa baada ya kuona analala na wao kwa mabalozi na kula nao, huku akisikiliza kero, mbinu ambayo ilimsaidia kupunguza upinzani Pangani.

Uenyekiti wa CCM wilaya aliutumikia kwa miaka mitatu tu kuanzia 2019 mpaka 2022 na baadaye ulianza mchakato wa kugombea nafasi ya mwenyekiti wa CCM mkoa na akaamua kuingia huko.

Anasema alipochukua fomu na jina lake kurudi kati ya majina matatu likiwemo la aliyekuwa mwenyekiti wa wakati huo, Henry Shekifu, baada ya uchaguzi aliibuka mshindi, akipata kura 373 kati ya 400.

Mwenyekiti Rajabu anasema kilichomfanya kugombea nafasi ya juu zaidi ni kitendo cha kusikia mara kwa mara kwamba Tanga ni mkoa ambao, upo nyuma kimaendeleo, hivyo dhamira yake ni kutaka kuona mabadiliko kuamsha mkoa kiuchumi.

Nyota ya Rajab kisiasa inazidi kung’’ra. Hivi karibuni, Rajabu alichaguliwa na Kamati Kuu ya CCM kuwa mjumbe wa kamati hiyo, baada ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kupendekeza jina lake, suala ambalo hata yeye lilimshtua.

Anasema ilimchukua takribani wiki nzima kuwaza imekuwaje hadi jina lake kutajwa kuchukua nafasi hiyo wakati wapo wanachama wenye majina makubwa. Anasema alithibitisha kwenye kateuliwa baada ya kuhudhuria vikao kadhaa na kuamini kweli imetokea.

Kutokana na nafasi alizoshika Rajabu hadi sasa na uteuzi huo wa mwisho, baadhi ya makada wa CCM wameanza kumtaja kwamba, anaweza kuwa miongoni mwa wanaofikiriwa kurithi nafasi ya makamu mwenyekiti wa CCM, iliyo wazi wazi baada ya Abdulrahman Kinana kuachia ngazi.

Makada hao wanamuona Rajabu kama mtu sahihi kutokana na aina ya uendeshaji wa siasa zake, utulivu, kuwa karibu na wananchi na muwazi, sifa ambazo wanaamini anapaswa kuwa nazo makamu mwenyekiti.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kauli za makada wa chama chake kuwa naye anatajwa kumrithi Kinana alisema: “Wanaotajwa wapo wengi sio mimi peke yangu, ila sipendi kuzungumzia hicho kitu kwa sababu hata nafasi ambazo nilikuwa nikiziomba nilikuwa naangalia kwamba kile nina uwezo nacho na nitaweza kufanya.”

Mwenyekiti huyo anasema kwa sababu akili yake ilikuwa kusukuma maendeleo ya Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Serikali, yapo baadhi ya malengo walioweka kupitia kwa viongozi waliopita na yeye kwa sasa yamefanikiwa.

Moja ya malengo ni kuboreshwa kwa Bandari ya Tanga na anasema mpaka sasa Serikali imeshatoa Sh429.1 bilioni kwa ajili hiyo ili kuongeza tija kwa uchumi wa wakazi mkoani humo.

Related Posts