RC KUNENGE -PWANI KUSIMAMIA MAONO YA RAIS DKT SAMIA KUVUTIA WAWEKEZAJI KWA WINGI

 

 

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani 2, Novemba,2024

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameeleza mkoa huo utaendelea kusimamia maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha unavutia wawekezaji kwa wingi.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alipotembelea kiwanda cha Goodwill kilichopo Mkuranga, Kunenge alisema, uwekezaji huo una faida kubwa kiuchumi na unaleta heshima kwa taifa, kwani bidhaa zinazotengenezwa zinabeba chapa ya “Made in Tanzania.”

Kunenge alisisitiza ,Mkoa wa Pwani una viwanda vingi vinavyochangia uchumi wa nchi na kwamba, kwa kiasi kikubwa, soko kuu la bidhaa hizo ni Dar es Salaam.

 “Tutahakikisha tunalinda na kuimarisha mazingira ya uwekezaji, ili bidhaa zinazozalishwa ziwe na mchango chanya kwa uchumi wa taifa na heshima ya Tanzania kimataifa,” alieleza Kunenge.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu na Mkoa wa Pwani si tu katika nyanja ya viwanda bali pia katika sekta zingine muhimu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Chalamila alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, akitolea mfano kiwanda cha Goodwill kinachomilikiwa na mwekezaji kutoka China, kama ishara ya juhudi kubwa za serikali za kuvutia wawekezaji nchini.

Alikipongeza pia kiwanda cha Goodwill kwa kutoa ajira kwa wazawa na akatoa rai kwa kiwanda hicho kinachozalisha vigae (tiles) kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu pamoja na kurudisha sehemu ya faida kwa jamii kupitia uwajibikaji wa kijamii (CSR).

 “Uwepo wa viwanda kama Goodwill ni muhimu kwa kuimarisha uchumi na kuleta ajira, hivyo tutahakikisha ushirikiano wetu na Mkoa wa Pwani unaimarika kwa masilahi ya wote,” alisema Chalamila.

Ushirikiano wa mikoa hii miwili unalenga kuhakikisha kuwa viwanda na wawekezaji wanapata mazingira mazuri ya kufanyia biashara, jambo linalosaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na ustawi wa jamii katika maeneo yote mawili.

 

Related Posts