WAKATI Singida Black Stars ikitarajia kuingia kwenye mchezo wa leo, Jumamosi dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kwa lengo la kurejea kwenye wimbi lao la ushindi, wagosi wa Kaya wao hesabu zao ni kuendeleza walichoifanya Kagera Sugar.
Singida BS ambayo imetoka kupoteza kwenye mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Yanga, ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 22, Coastal Union yenyewe ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 11.
Kocha Patrick Aussems wa Singida Big Stars ameonyesha dhamira ya kurejea kwenye ushindi, akiwataka wachezaji kucheza kwa nguvu na kuonyesha nidhamu ya juu katika safu ya ulinzi, jambo ambalo lilikuwa changamoto kwenye mchezo uliopita.
“Baada ya kupoteza dhidi ya Yanga, tunahitaji kushinda kesho (leo) ili kujirejesha kwenye hali nzuri. Coastal ni timu yenye nidhamu, lakini tunahitaji pointi tatu, na wachezaji wangu wamejiandaa kwa changamoto hiyo,” alisema Aussems.
Ushindi kwa Singida sio tu utarejesha morali ya timu baada ya kipigo cha Yanga, bali pia utaimarisha nafasi yao. Aussems anaingia kwenye mchezo huo akitegemea nyota wake kama vile Marouf Tchakei, Elvis Rupia, Ande Koffi, Anthony Tra Bi Tra na Emmanuel Kayekeh ambao wamekuwa na msimu mzuri, na ana matumaini kwamba wataonyesha uwezo wao kwenye mchezo huu muhimu.
Kwa upande wa Coastal Union, mchezo huu ni fursa kwa kocha wao mpya Juma Mwambusi, ambaye amechukua nafasi ya kuongoza timu akiwa na dhamira ya kuipandisha kwenye nafasi za juu.
Mwambusi anaingia kwenye mchezo huu akitambua kuwa alama yoyote itakuwa ya thamani kwao. Hata sare inaweza kuimarisha hali ya Coastal na kuwapa ari ya kuendelea kupanda kwenye msimamo wa ligi. Wanaingia kwenye mechi hii wakitegemea uzoefu wa wachezaji kama Mbaraka Yusuph, mshambuliaji mwenye uwezo wa kuleta matokeo katika mashambulizi ya haraka.
Mwambusi, akiwa na mkakati wa kucheza kwa tahadhari na kujilinda vizuri, anataka timu yake iwe na nidhamu ya hali ya juu.
“Najua tunakutana na timu yenye nguvu, lakini wachezaji wangu wamejiandaa kwa hali yoyote. Lengo letu ni kupata matokeo mazuri, na nadhani tunaweza kufanikisha hilo kwa nidhamu na umakini wa hali ya juu,” alisema Mwambusi.
Mbinu zinazotarajiwa kuonekana kwenye mchezo huu ni mchanganyiko wa ushambuliaji wa moja kwa moja kutoka kwa Singida na mpango wa Coastal wa kutumia mashambulizi ya kushtukiza.
Mbali na mchezo huo, Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa maafande wa Tanzania Prisons kucheza dhidi ya Kengold.