Stars hairudii makosa Dar | Mwanaspoti

TAIFA Stars ina uhakika wa kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza kwenye adhi ya nyumbani (CHAN) 2025, sambamba na Kenya na Uganda, lakini hiyo haiwafanyi wabweteke wakati kesho jioni watakapovaana na Sudan katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya mechi za kuwania fainali hizo.

Stars ililala kwa bao 1-0 ugenini wikiendi iliyopita huko Mauritania, lakini leo itakuwa na nafasi ya kulipa kisasi wakati timu hizo zitakaporudiana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na mshindi wa jumla atasonga mbele raundi ya pili kuvaana na Ethiopia iliyopewa ushindi wa chee kutokana na Eritrea kujitoa.

Mchezo huo hautakuwa na kiingilio baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusema mashabiki wataingia bure uwanjani, kuiunga mkono Stars ili iweze kulipa kisasi dhidi ya Sudan na kutinga raundi inayofuata dhidi ya Waethiopia.

Tangu irejee nchini kutoka Mauritania, Stars ilikuwa ikijifua kwenye viwanja wa TRA, Kurasini na baaade KMC uliopo Mwenge kujiweka fiti kwa mchezo huo na mapema kocha mkuu wa timu hiyo, Bakar Shime pamoja na wachezaji walisema wamejianda vya kutosha kuhakikisha wanapata matokeo mazuri nyumbani.

“Ni mchezo mgumu na hasa baada ya kupoteza ugenini, Wasudan watakuja wakitaka kulinda ushindi wao nasi tukitaka kulipa kisasi ili tusonge mbele kwa hatua inayofuata, bahati tumeshagundua makosa na tumejipanga kufanya vizuri na tupo nyumbani,” alisema Shime.

Tanzania, Kenya na Uganda ndio wenyeji wa fainali hizo za CHAN zikazofanyika kabla ya Afcon 2025 zitakazopigwa Morocco, kisha nchi hizo tatu za Afrika Mashariki kuja kuanda Afcon 2027.

Stars itaendelea kuwategemea wachezaji wengi wa timu ya Vijana U20 iliyobeba ubingwa wa Cecafa na wazoefu kadhaa wa Ligi Kuu.

Related Posts