Tanzania yapanda viwango vya uhuru wa habari

Dar es Salaam. Tanzania imepanda katika viwango vya uhuru wa habari kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka huu.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Waandishi wa Habari wasio na Mipaka (RSF).

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania ina kila sababu ya kuongeza nguvu ya kuwalinda waandishi wa habari dhidi ya madhila kutokana na kuongezeka dhidi yao kwa mwaka huu 2024 ukilinganisha na miaka miwili iliyopita.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura katika taarifa kwa umma aliyoitoa leo Novemba 2, 2024 katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya waandishi wa habari (IDEI).

Sungura pia ni Mwenyekiti wa umoja wa haki ya kupata taarifa nchini Tanzania (CoRI) na Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Usalama wa waandishi wa habari wakati wa migogoro na dharura.

Amesema kati ya mwaka 2012 hadi Oktoba 2024 waandishi wa habari 316 walipatwa na madhila nchini, 44 kwa mwaka huu pekee ikiwa ni sawa na madhila 33.

Madhila hayo amesema yanahusisha kukamatwa kwa waandishi 31, vitisho (8), kutekwa na watu wasiojulikana (1), onyo kwa vyombo vya habari (4), chombo cha habari kufungiwa (4), kipindi kukatishwa kikiwa hewani (1), kusumbuliwa (1), kunyimwa taarifa (1), uhuru wa mahakama kuingiliwa (1) na kunyang’anywa vifaa (1). Kati ya hayo amesema wanaume ni 36 na wanawake ni wanane.

Sungura amesema mwaka 2022 madhila 19 yalirekodiwa, mwaka jana (23) na mwaka huu hadi leo Novemba 2, mwaka huu (33) yamerekodiwa.

“Madhila husika ni ya waandishi wa habari kukamatwa, kupewa vitisho, vyombo vya habari kupewa onyo, kufungiwa kufanya kazi, kuingilia uhuru wa mahakama na kuahirisha kipindi kwenda hewani,” amesema.

Sungura amesema CoRI inaunga mkono mazungumzo kati ya Serikali na wadau wa habari katika kujenga mwafaka wa kukabiliana na ukatili dhidi ya waandishi wa habari hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuhusu ukatili dhidi ya waandishi wa habari, kiwango cha ukatili ni kikubwa.

Kati ya mwaka 2006 hadi 2024 zaidi ya waandishi 1,700 wameuawa duniani na kesi za mauaji hayo asilimia 90 hazijatatuliwa mahakamani.

“Sote tunajua umuhimu wa waandishi wa habari, hivyo ukatili dhidi yao una madhara makubwa katika kukuza na kulinda demokrasia ya kila taifa duniani,” amesema Sungura.

Amesema Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA) na CoRI, kwa pamoja yanapinga ukatili dhidi ya waandishi wa habari kote duniani.

Related Posts