Dar es Salaam. Wengi wamekuwa wakijiuliza ni noti zipi ambazo zimetangazwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwa zitaondolewa kwenye mzunguko wa matumizi kati ya Januari na Aprili mwakani.
Hivi karibuni Bot ilitangaza kuziondoa noti za Sh20, Sh200, Sh500, Sh1,000, Sh2,000, Sh5,000 na Sh10,000 zilizotolewa kuanzia mwaka 1985 hadi 2003, pamoja na noti ya Sh500 iliyotolewa mwaka 2010, kama ambavyo zinaonekana kwenye video.
Taarifa hiyo ya Oktoba 24, 2024 iliyosainiwa na Gavana wa benki hiyo, Emmanuel Tutuba, ilihusisha Tangazo la Serikali Na. 857 na 858 lililochapishwa Oktoba 11, 2024 ambalo limetoa wito wa kuwasilisha, kuweka au kubadilisha, na kusitisha matumizi ya noti za zamani.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kazi hiyo itaendelea kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari 6, 2025 hadi Aprili 5, 2025, noti hizo zitakapositishwa kuwa sarafu halali.
“Zoezi la ubadilishwaji linatarajiwa kuanza Januari 6, 2025 hadi Aprili 5, 2025 kupitia Ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imesema matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia Aprili 6, 2025.
Akifafanua zaidi kuhusu hatua hiyo Kaimu Mkurugenzi wa usimamizi wa Sarafu wa BoT, Ilulu Ilulu anasema zoezi hilo si geni kwa mamlaka hiyo yenye jukumu la pekee la kuchapisha noti na kuzisambaza nchini Tanzania kwa sheria ya mwaka 2006 sura ya 197.
“Kupitia kifungu cha 28 (2) na (3) ya Sheria hiyo, Benki Kuu imepewa mamlaka ya kusitisha uhalali ya fedha itakazozianisha kadri itakavyoona inafaa kwa kuchapisha tangazo katika Gazeti la Serikali,” anasema.
Ilulu anasema inapotokea kusitisha uhalali wa noti fulani wananchi hupewa muda maalumu wa kuzibadilisha kabla ya kusitisha uhalali huo na hupewa fursa ya kubadilisha noti husika kwa kupewa kiwango kile kile.
Alisema kabla ya tangazo la mwezi uliopita, BoT iliwahi kutoa tangazo kama hilo mwaka 1977 kusitisha noti ya Sh100 iliyochapishwa kuanzia mwaka 1966 hadi 1977 na tangazo la mwaka 1979 la kuziondoa kwenye mzunguko noti za Sh10, 20 zilizochapishwa mwaka 1979.
Tangazo lingine ni la mwaka 1980 lililoziondoa kwenye mzunguko noti za Sh5 na Sh20 zilizochapishwa kati ya mwaka 1966 mpaka 1980 na tangazo la mwaka 1995 lililoziondoa kwenye mzunguko noti za Sh50 na Sh100 zilizochapishwa kati ya mwaka 1979 mpaka mwaka 1995.
Akizungumzia hatua hiyo, mchambuzi wa masuala ya uchumi ya fedha na benki Dk Thobias Swai amesema hatua hiyo inachukuliwa ili watu waliotunza fedha hizo wakijua zina thamani wazibadili.
“Ni utaratibu wa kawaida kwenye masoko ya fedha kutangaza noti ambazo zimepitwa na wakati ili kama mtu alitunza akijua zina thamani asipate hasara na anapewa thamani yake ileile, ni utaratibu wa kawaida,” anasema Dk Swai.