Dar es Salaam. “Maisha ya Mwanadamu ni kama Hadithi tu, Basi ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa” Hii ni kauli iliyowahi kutolewa na hayati Ali Hassan Mwinyi, ambaye alikuwa Rais wa awamu ya pili. Kauli hiyo inaendana na kilichoachwa na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Kipenka Msemembo Mussa (69) aliyefariki dunia Jumamosi Novemba 2, 2024, katika Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Jaji Kipenka ameacha hadithi nzuri inayopaswa kusimuliwa baada ya kifo chake hasa usimamizi wake katika kutoa haki.
Jaji Kipenka alilitumikia Taifa maeneo mbalimbali katika mihimili yote mitatu ya dola, yaani Serikali, Mahakama na Bunge. Huku muda mwingi wa utumishi wake akiutumia katika sekta ya haki serikalini na mahakamani.
Serikalini Jaji Kipenka alihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwamo Wakili wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Haki za Binadamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wa mhimili wa Bunge, Jaji Kipenka aliwahi kuwa Katibu wa Bunge kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2004.
Katika mhimili wa Mahakama alihudumu katika nafasi ya ujaji, akianza na Jaji wa Mahakama Kuu kuanzia mwaka 2004 alipoteuliwa katika nafasi hiyo mpaka 2012 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani hadi mwaka 2019 alipostaafu utumishi huo kwa mujibu wa sheria.
Mbali na majukumu yake ya kila siku katika utumishi wake hususan ya kuendesha kesi (akiwa Wakili wa Serikali) na kuamua kesi mbalimbali pia Jaji Kipenka alitumika katika Tume mbalimbali za uchunguzi wa haki jinai.
Hizi ni Tume za Rais zilizoundwa kuchunguza mazingira ya matukio mawili tofauti ya mauaji yaliyotikisa nchini kila moja kwa wakati wake.
Tume hizo ni pamoja na ya mauaji ya aliyekuwa Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe aliyeuawa na askari Polisi Juni 30, 1996, kwa madai ya kufananishwa na mtuhumiwa wa wizi wa magari waliyekuwa wakimtafuta.
Katika Tume hiyo Jaji Kipenka alikuwa Katibu wa Tume na kufuatia uchunguzi huo, watuhumiwa wawili, Koplo Juma Mswa na Konstebo Mkataba Matiku walishtakiwa kwa kesi ya mauaji ya kukusudia.
Mwaka 1998 baada ya kesi kusikilizwa walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa lakini baadaye wakati wa utawala wa Rais Kikwete aliwabadilishia adhabu kutoka kunyongwa na kuwa kifungo cha miaka miwili, ambayo waliimaliza mwaka 2011 na kuachiwa huru.
Mauaji ya wachimba madini
Tume nyingine ni ile ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, mkoani Morogoro na dereva teksi mmoja mkazi wa Manzese Dar es Salaam waliyekuwa wamemkodi kwa ajili ya mizunguko yao jijini Dar es Salaam, ambayo Jaji Kipenka alikuwa mwenyekiti.
Wachimba madini hao Sabinus Sabinu Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake Ephraim Chigumbi pamoja na mwenzao Mathias Lunkombe na dereva teksi Juma Ndugu, waliuawa Januari 14, 2006 na askari Polisi waliokuwa doria tarehe hiyo.
Tume hiyo iliundwa na Rais Kikwete kwa ajili kuchunguza ukweli mauaji hayo, baada ya Mwananchi kuibua utata kuhusiana na mauaji ya wachimba madini hao.
Jeshi kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi Dar es Salaam, ambaye pia alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe liliutangazia umma kuwa wafanyabiashara hao walikuwa ni majambazi.
ACP Zombe alieleza majambazi (wauza madini hao) hao walihusika katika matukio mbalimbali ya uporaji eneo la Kariakoo na pesa katika gari la mauzo la kampuni ya Bidco, katika Barabara ya Sam Nujoma eneo la Konoike.
Hivyo alieleza waliuawa wakati wakirushiana risasi na akari waliokuwa doria, wakikaribia kukimbia kwa kuruka ukuta wa Shirika la Posta, Sinza.
Hata hivyo, Mwananchi baada ya kufuatilia tukio hilo liliibua taarifa kinzani na zilizotolewa na Jeshi la Polisi, kuwa hao waliouawa walikuwa ni wachimba madini na kwamba walikamatwa Sinza nyumbani kwa mwenzao, wakafungwa pingu bila ukinzani na Polisi wakaondoka nao wakiwa wazima.
Kutokana na mwangwi mkubwa wa kelele zilizopazwa na ndugu wa marehemu na wadau mbalimbali kufuatia taarifa hizo ndipo Januari 23, 2006, Rais Kikwete akaunda tume hiyo kuchunguza ukweli wa mauaji hayo na akamteua Jaji Kipenka kuwa mwenyekiti.
Katika hadidu za rejea tano ambazo tume hiyo ilipewa ilitakiwa kuchunguza chanzo na mazingira ya mauaji ya watu hao wanne waliouawa Sinza (kama ilivyodaiwa na Polisi), na kuchunguza ukweli wa maelezo ya Jeshi la polisi kuwa watu hao walikuwa wamepora fedha (za kampuni ya Bidco).
Nyingine zilikuwa ni kuchunguza na kutambua majina ya marehemu, walikokuwa wakiishi na kazi zao; uhalali wa nguvu iliyotumika na ya mwisho ilikuwa ni maoni na ushauri kwa tukio zima.
Tume hiyo ilipewa siku 24, ilianza kazi yake Januari 25,2006 kwa kikao cha kuweka mpango kazi, ambapo ilitoa samansi kwa askari polisi waliohusika kuwakamata wachimba madini hao na kutoa matangazo kwa mtu yeyote aliyekuwa na taarifa za mauaji hayo kufika mbele ya tume.
Tume hiyo ilianza rasmi kazi ya kuwahoji na kupokea maelezo ya mashahidi kuanzia Januari 26 kwa kuandika na kurekodiwa kwa kanda za sauti (tape recorders).
Tume hiyo ilitembelea maeneo matatu yaliyokuwa yametajwa kuhusika katika tukio, ikianzia Barabara ya Sam Nujoma mahali lilikodaiwa kutokea tukio la uporaji wa fedha za Bidco, mkabala na kampuni ya ujenzi ya Konoike.
Eneo lingine ni katika ukuta wa Posta Sinza na eneo la Sinza C nyumbani kwa mchimba madini wenzao na marehemu walikokamatiwa.
Kisha Tume ilikwenda Mahenge ambako wachimba madini hao walikuwa wakifanyia shughuli zao.
Kwa ujumla tume hiyo ilichukua ushahidi wa mashahidi 90 kutoka Dar es Salaam, Mahenge na wawili kutoka Arusha na Februari 17, 2006 ilikabidhi taarifa yake kwa Rais Kikwete.
Akisoma taarifa hiyo, Jaji Kipenka alisema katika uchunguzi wake, tume ilibaini kweli waliouawa walikuwa wafanyabiashara ya madini Mahenge.
Alisema kuwa walikuwa wamekuja kuuza madini yao na kwamba walitiwa mbaroni eneo la Sinza C, bila ghasia yoyote, wakafungwa pingu kabla ya kuondoka nao.
Jaji Kipenka alisema maofisa wa Polisi waliowatia mbaroni Sinza, lazima walikuwa wana jambo la kufanya kuhusu vifo hivyo.
Hivyo alisema tume inapendekeza kwamba sheria inapaswa kuchukua mkondo kwa wale ambao wanawajibika na vifo hivyo na kwamba inapendekeza hatua za kinidhamu kwa Kaimu RPC (ACP Zombe).
Kutokana na taarifa hiyo askari na maofisa wote wa Polisi waliohusika katika tukio hilo walikamatwa kwa nyakati tofauti na kushtakiwa kwa mauaji ya wachimba madini hao na dereva teksi, akiwemo ACP Zombe.
Wengine walikuwa ni, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni na askari polisi 11.
Kwa mujibu wa ushahidi katika kesi hiyo, askari hao baada ya kuwakamata wachimba madini hao waliwapeleka katika Msitu wa Pande, Wilayani Kinondoni Dar es Salaam, ambako waliwaua kwa kuwapiga risasi mmoja mmoja wakiwa wamelazwa chini kifudifudi.
Hata hivyo, Mahakama Kuu katika hukumu yake ya Agosti 17, 2009 iliyotolewa na Jaji Salim Masatti aliyesikiliza kesi hiyo iliwaachia huru wote kwa maelezo kuwa ushahidi ulionyesha aliyewafyatulia risasi ni Koplo Saad Alawi, ambaye hakuwa miongoni mwa washtakiwa na hajulikani alikokuwa.
Hivyo Jaji Masatti aliamuru Koplo Saad atafutwe na ashtakiwe kwa mauaji hayo.
Hata hivyo, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani ambayo katika hukumu yake Septemba 16, 2016 baada ya kuchambua ushahidi ilimtia hatiani SP Bageni baada ya kuridhika kuwa Koplo Saad alitekeleza mauaji hayo kwa amri na usimamizi wake na ikamuhukumu adhabu ya kunyongwa.