HOMA ya Guru Nanak Rally, ambayo ni raundi ya mwisho ya mbio za magari ubingwa wa taifa, inazidi kupanda huku washiriki wakizidi kujitokeza kabla ya mbio hizo kutimua vumbi Novemba 16 na 17 mwaka huu.
Kutoka jijini Dar es Salaam, timu ya Amapiano inasema imepania kuweka rekodi tatu katika mbio hizi za funga msimu ambazo zitachezwa katika eneo la Makuyuni, takribani kilometa 80 magharibi mwa jiji la Arusha.
Timu hii inayoundwa na madereva Ethan Taylor, Isack Taylor, Charles Bicco na msoma ramani David Matete, itakuwa ni moja ya washiriki wa raundi ya nne na imejizatiti kutoa upinzani kwa madereva nyota wa ndani na nje ya nchi, kwa mujibu wa msemaji wake David Matete.
Akizungumza na Mwanaspoti mwishoni mwa juma, Matete amesema Ethan Taylor mwenye miaka 18 atakuwa ni mshiriki mwenye umri mdogo kuliko wote katika mashindano hayo wakati Isack Taylor atakiwa akiwania kuandika historia ya kushiriki na Toyota Celica GT4, ambayo ilikuwa ni gari bora ya zamani (classic) miongo minne iliyopita.
“Pamoja na hao wawili kuwania rekodi katika vitengo vya umri na gari iliyokuwa na ubora uliotukuka, mimi na Bicco tutakuwa tukijaribu kuirudisha katika chati gari aina ya Subaru 12 ambayo ilikuwa maarufu katika miaka ya awali ya 2000,” alifafanua Matete.
Matete alisema Ethan licha ya umri wake mdogo ataingia na Subaru Gc 8 ambayo ni ni toleo la miaka ya tisini.
“Tunajiandaa vyema na nina imani tutafanya vizuri, na tunawashukuru wadhamini wetu Molas Lubes na Luquimoly kwa kutuwezesha kushiriki katika mashindano haya na yaliyopita,” alisema Matete.
Mashindano haya yanaandaliwa na klabu ya mbio za magari ya Arusha (AMSC), na kwa mujibu wa mwenyekiti wake, Goodluck Mariki yataanza kwa mbio fupi za Super Special Stage katika maeneo ya Mswakini na Naitolya.
Mariki alisema mbio hizo za siku mbili zitakuwa za umbali wa kilometa 217.
Alisema kuwa siku ya kwanza, Novemba 16 mwaka huu, magari yatakimbia kilometa 67 kabla ya kumaliza na kilometa 150 siku ya pili, Novemba 17 mwaka huu.
Mbali ya madereva hawa kutoka Dar es Salaam, kutakuwapo pia na timu ya madereva mahiri kutoka Kenya, Uganda, Zambia na kwingineko Tanzania.