WANA fainali ya Ngao ya Jamii kwa wanawake, Yanga Princess, wamedhamiria kufanya makubwa msimu huu ikiwamo kubeba taji la Ligi Kuu ya Wanawake kwa mara ya kwanza ikiwa ndio ndoto yao.
Chini ya kocha aliyerejea msimu huu, Edna Lema ‘Mourinho’, Yanga Princess ilitinga fainali ya Ngao ya Jamii kwa kumtoa mtani wake, Simba Queens kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare ya 1-1 na kwenye ligi tayari imecheza mechi mbili ikitoka 0-0 na Alliance na 1-1 dhidi ya Bunda Queens.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lucy Mwenda alisema viongozi wa klabu hiyo wanafanya kila kitu kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na pengine hata kuchukua ubingwa.
Aliongeza kuwa kwa sasa timu hiyo inapewa karibu mahitaji yote kama yale wanayopata timu kubwa ili mambo yaende sawa.
“Leo hii tunapata nafasi ya kusafiri kwa ndege kwenda kwenye mechi za ndani, jambo hili limeweka historia kwa klabu yetu na lengo ni kuepusha uchovu wa barabarani kama wachezaji na sisi tunafanya jitihada kuhakikisha hatuwaangushi viongozi,” alisema Mwenda na kuongeza:
“Nje na hayo kuna vitu kama kuahidiwa bonasi endapo tutashinda mechi, hilo linaonyesha ni wazi viongozi wamedhamiria kuleta mageuzi kwenye soka la wanawake na matamanio yetu makubwa kufanya vizuri kama timu kubwa.”