Diaspora kutuma fedha moja kwa moja Tanzania

Dar es Salaam. Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) sasa wataweza kutuma fedha moja kwa moja nchini, baada ya kuanzishwa kwa programu ya kifedha kwa waafrika ijulikanayo kama Kuda.

Kuanzishwa kwa programu hiyo huenda kutachochea kuongezeka kwa kiwango cha fedha kinachotumwa Tanzania kwa ajili ya shughuli mbalimbali, ikiwemo uwekezaji.

Programu hiyo inatangazwa baada ya Kuda kupewa leseni ya Mtoa Huduma za Malipo (PSP) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Kuda Technologies, Babs Ogundeyi amesema kupata leseni ya PSP Tanzania ni hatua kubwa kwa kampuni hiyo katika kupanua wigo wa Bara la Afrika katika uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi na familia kwa ujumla.

“Watanzania wanaoishi nchi kama vile Uingereza, Umoja wa Ulaya, Marekani, na Canada wanaweza kutumia huduma hii kwa gharama nafuu kupitia njia mbalimbali za malipo kama vile kadi, pesa kwa njia ya simu, uhamisho wa benki, USSD na EFT kutokana na ukuaji wa teknolojia,” amesema Ogundeyi katika taarifa yake kwa umma jana, Jumamosi Novemba 2, 2024.

Amesema Tanzania ni soko muhimu katika kuwahudumia watu wanaoshi ughaibuni na kuwaunganisha na familia zao katika upatikanaji wa huduma za kifedha.

“Leseni tuliyopewa na BoT inatuwezesha kutoa huduma za kifedha za uhakika kwa gharama nafuu, ili kuwawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki katika ujenzi wa Taifa kupitia uwekezaji na maendeleo ya familia zao,” amesema Ogundeyi.

Amesema upatikanaji wa huduma hiyo si muhimu kwa Tanzania tu, bali Bara la Afrika kwa ujumla.

Kuanza kwa huduma hiyo utawawezesha wana daispora kutuma fedha kwa urahisi kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile uwekezaji katika biashara mbalimbali na huduma za kijamii.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, uhitaji wa kutuma fedha kutoka nje ya nchi unaofanywa na Watanzania wanaoishi ughaibuni umekuwa ukiongezeka na kwa mwaka 2021, kiasi cha fedha zilizotumwa Tanzania kilifikia Sh1.53 trilioni.

“Tumejidhatiti kuwawezesha Watanzania waishio ughaibuni na kusaidia ukuaji wa kiuchumi wa kanda kwa kutoa huduma za kutuma fedha kwa usalama na urahisi ambazo zinaimarisha ushirikishwaji wa kifedha,” amesema.

Programu hiyo inazinduliwa pia wakati ambao taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu mwenendo wa uhamiaji duniani (KNOMAD, 2024) ikionyesha Watanzania bado wanatuma kiasi kidogo cha fedha kutoka sehemu walipo.

Ripoti hiyo inazitaja nchi za Nigeria na Kenya kuongoza barani Afrika kwa kupokea kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa raia wao walioko ughaibuni (Diaspora).

Ripoti hii inaonyesha kuwa hadi Desemba 2023, Diaspora wa Nigeria walituma Dola bilioni 19.5 (Sh53.04 trilioni) kwa nchi hiyo, ikiwa ndio kiwango kikubwa zaidi barani Afrika. Kiasi hicho ni zaidi ya robo ya jumla ya Dola bilioni 54 zilizopokewa na nchi 49 za ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa upande wa Kenya ilipokea makadirio ya dola bilioni 4.2 za Marekani (Sh11.42 trilioni), huku Tanzania ikipokea makadirio ya Dola milioni 700 (Sh1.9 tilioni) kutoka kwa diaspora mwaka 2023.

Related Posts