Geita Gold gari limewaka, Arusha kuna Dabi ya Monduli

LICHA ya kuanza kwa kuchechemea katika Ligi ya Championship, Geita Gold imejipata na gari limewaka huku winga wa timu hiyo, Yusuph Mhilu akitoboa siri kuwa wachezaji wameelewa, kupata muunganiko na tayari benchi la ufundi limeshapata kikosi cha kwanza na kujua namna ya kuipanga timu yao.

Timu hiyo iliyoshuka kutoka Ligi Kuu Bara msimu uliopita, inaongoza Ligi ya Championship ikiwa na alama 14 baada ya kushinda michezo minne na sare moja, ikifunga mabao nanane na kuruhusu moja huku ikiwa haijapoteza mchezo. Mtibwa Sugar ni ya pili na pointi 13 na TMA Stars ni ya tatu na alama 12.

Mhilu aliliambia Mwanaspoti kuwa mwanzo walipata ugumu kutokana na ugeni wa wachezaji na benchi la ufundi kutoelewana lakini kwa sasa wamejipata na wanataka kuhakikisha wanaokota alama tatu katika michezo yao.

Mhilu aliyefunga bao katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Kiluvya United, alisema ni msimu wake wa kwanza kwenye michuano hiyo na anaamini ubora wa kikosi chao utamsaidia kurejesha makali yake na kucheza tena Ligi Kuu Bara kama ambavyo mashabiki wamemzoea.

“Mwanzoni ilikuwa inampa mwalimu ugumu kutambua wachezaji wake ni wa aina gani na atawatumia vipi ndiyo maana mechi za mwanzo hatukucheza vizuri kwa sababu maandalizi yake yalikuwa magumu mtu kumuelewa mwalimu mapema,” alisema Mhilu na kuongeza;

“Baadaye tukamzoea mwalimu na kuelewa anachokitaka na muunganiko aliokuwa anautafuta umeshapatikana na kombinesheni ya timu yetu imefanikiwa, tunacheza kwa umoja na kujitolea kwa ajili ya timu tukiwa uwanjani na tunatengeneza nafasi za kufunga mabao.”

Akizungumzia maandalizi ya mchezo wa leo Jumapili dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita, Mhilu alisema mipango iko vizuri wanajiandaa kuendeleza wimbi la ushindi nyumbani ili wasitoke kileleni kwani wameshatambua ligi inavyochezwa na umuhimu wa kutumia vyema uwanja wa nyumbani.

“Kila timu inatamani ishinde kwake na sisi tutafanya kila jitihada kupata ushindi ili kupata morali ya kwenda kucheza mechi za nje. Maandalizi yako vizuri mwalimu amefanyia marekebisho matatizo yaliyojitokeza katika mechi zilizopita kwahiyo tuna imani Jumapili (leo) tutashinda,” alisema Mhilu.

Mechi nyingine ya leo ya ligi hiyo ni Dabi ya Monduli kati ya mafande wa Mbuni na TMA Stars itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

TMA Stars imeshinda mechi mbili nyumbani, huku ugenini ikishinda moja na kutoka sare tatu, wakati Mbuni  imeshinda mechi moja pekee, sare tatu na kupoteza mbili huku ikifunga mabao manne na kufungwa matano na kwa  nyumbani imepoteza moja sawa na sare mbili, ugenini ikishinda moja na kutoka sare mbili.

Akizumgumza mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, kocha wa Mbuni FC, Leonard Budeba alisema kikosi chake kiko katika hali nzuri kuhakikisha kinashinda na kupata alama zote tatu.

“TMA ni timu ngumu najua na mchezo hautakuwa mrahisi ila tumejipanga kushinda na kuondoka na alama zote tatu ambazo ndio malengo yetu ya mchezo huu,” alisema Budeba.

Kocha wa TMA Stars, Maka Mwalwisi alisema tayari makosa ambayo yalijitokeza katika mechi mbili za mwisho ambazo walitoka sare amefanyia kazi kuhakikisha katika mchezo wa leo hazijitokezi na kuwapa urahisi ya kupata matokeo.

Alisema kwao hakuna mechi rahisi, kila mchezo ni fainali, maandalizi ambayo wanafanya kwa timu zote ni sawa hivyo kabla ya mchezo wa leo tayari alishawandaa wachezaji wake vyema kisaikolojia.

Related Posts