Dar es Salaam. Hitilafu iliyotokea katika mfumo ya uendeshaji wa treni ya umeme imesababisha mvurugiko wa ratiba za treni hiyo jambo ambalo limewafanya baadhi ya abiria kukwama katika stesheni tofauti.
Abiria hao waliokuwa wakisafiri kwa nyakati tofauti walijikuta njia panda baada ya muda ambao walipaswa kusafiri kufika lakini safari hazikufanyika.
Kufuatia suala hilo, TRC kupitia taarifa yao kwa umma imeomba radhi huku ikiweka bayana kuwa mafundi wako eneo la tukio wanafanyia kazi changamoto hiyo.
“Shirika la reli Tanzania (TRC) linaomba radhi kwa abiria wa treni ya mchongoko (emu) walioanza safari yao Dar es Salaam kwenda Dodoma saa 2:00 asubuhi na kusimama ghafla saa 2:20 kati ya Pugu na Soga. Pia tunaomba radhi kwa abiria wetu wa treni ya saa 11:15 alfajiri kutoka Dodoma na treni ya saa 3:30 kutoka Dar es Salaam ikijumuisha safari nyingine za siku ya leo ambazo zimeathiriwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Treni ya mchongoko inakwama ikiwa ni siku ya tatu tangu ianze kufanya kazi ya usafirishaji abiria kati ya Dar es Salaam na Dodoma. Novemba Mosi, 2024 ndiyo ilianza rasmi kazi ikitokea Stesheni ya Magufuli mkoani Dar es Salaam hadi Stesheni Kuu ya Samia mkoani Dodoma.
Treni hiyo ina vichwa mbele na nyuma tofauti na treni zenye kichwa kimoja, huku ikibeba jumla ya abiria 589 na inatembea kwa mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa.
Endelea kufuatilia mwananchi kwa taarifa zaidi