Kikwete aguswa na mchango wa Sh1 bilioni za NMB kwa JKCI

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amepongeza juhudi za wadau wa afya nchini kwa kufanikisha uchangishaji wa Sh2.71 bilioni kwa ajili ya matibabu ya watoto 1,500 wanaokabiliwa na changamoto za  kugharamia matibabu ya ugonjwa wa moyo.

Katika kiasi hicho, Benki ya NMB ilichangia Sh1 bilioni zilizokusanywa kwenye hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Rais Kikwete alitoa pongezi hizo jana usiku, Novemba 2, 2024, kwenye hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa fedha hizo zitaongeza nguvu kwa Serikali katika kuboresha uwezo wa ndani wa kutibu maradhi ya moyo.

Hafla hiyo, iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa JKCI na Heart Team Africa Foundation (HTAF), ilikuwa na kaulimbiu isemayo; “Tia nuru, gusa moyo, toa matumaini kwa maisha ya watoto.” Rais Kikwete alisema gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi ni kubwa na ndio sababu iliyosukuma uanzishwaji wa JKCI, taasisi ambayo sasa inachukua jukumu kubwa la kutoa huduma za matibabu ya moyo nchini.

Alieleza kuwa Serikali inagharamia asilimia 70 ya matibabu, huku familia zikichangia asilimia 30 (Sh4 milioni), kiwango ambacho ni kikubwa kwa familia nyingi.

Kikwete alisifu pia michango ya wadau wa afya, akieleza kuvutiwa na msaada mkubwa wa NMB, ambayo imetoa Sh1 bilioni zilizotolewa na benki hiyo zinatarajiwa ambazo zinakwenda kuwasaidia watoto takribani 250 kati ya 1,500 wanaohitaji msaada, wakiwamo 500 ambao wanahitaji operesheni za haraka.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna kabla ya kukabidhi hundi, alimpongeza Rais Kikwete kwa maono yake ya kuanzisha JKCI ili kutoa suluhisho kwa Watanzania wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo.

Alisema NMB imetoa msaada huo kwa imani kwamba utawezesha wazazi ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya watoto wao. “NMB tutashirikiana na JKCI katika kutoa elimu kwa jami, ili kuongeza uelewa wa afya ya moyo,” alisema Zaipuna.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge alimpongeza Kikwete kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya afya wakati wa uongozi wake.

Dk Kisenge pia aliipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma na mifumo ya afya kwa kuungwa mkono na wadau.

“Tangu kuanzishwa kwa JKCI mwaka 2015, zaidi ya upasuaji 688,000 umefanyika na taasisi hiyo imekuwa mkombozi kwa nchi za Afrika Mashariki katika kukabiliana na changamoto za maradhi ya moyo,” alisema Dk Kisenge.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya HTAF na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu alitoa shukrani zake kwa Rais mstaafu Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya afya, akisema kuwa JKCI imekuwa kimbilio la wengi sio tu Tanzania, bali pia katika nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.

Related Posts