Kiungo Misri moto ni uleule

NYOTA wa Tanzania, Maimuna Kaimu ‘Mynaco’ ameendelea kuwa nguzo imara kwenye eneo la kiungo la Zed FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake wa Misri.

Ni msimu wa pili kwa Mynaco kucheza ligi hiyo ambayo msimu huu imeongezwa timu mbili, Pyramids na Al Ahly za wanawake.

Licha ya timu hiyo kuongeza nyota wapya wa kimataifa na kuongeza ushindani wa namba kikosini, Maimuna ameendelea kuonyesha kiwango bora msimu huu.

Mechi ya kwanza ya msimu ilikuwa dhidi ya Al Masry, Zed ikishinda mabao 4-0 na mechi ya pili ambayo pia Maimuna alicheza tena kwa dakika 90 dhidi ya Wadi Degla, timu yake ililala kwa mabao 3-2.

Na baada ya kumaliza majukumu ya timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Oktoba 31, akacheza mechi ya tatu ya ligi dhidi ya Al Maadi, Zed ikishinda mabao 6-0.

Ni wazi sasa nyota huyo ameiteka nafasi ya kiungo licha ya kujumuisha wachezaji wengi wa Misri kwenye eneo lake.

Akizungumza na Mwanaspoti juu ya kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho, alisema jambo kubwa linalombeba ni uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti kwenye eneo la kiungo.

“Nafikiri nimekuwa nikipata nafasi kubwa kwa sababu kila mechi kocha hunitumia katika nafasi tofauti ya kiungo kulingana na mechi na nimekuwa nikifanya vyema ndio maana kocha ananipa nafasi,” alisema Mynaco.

Related Posts