Kocha Transit Camp afichua jambo

KOCHA mkuu wa Transit Camp, Ally Ally amesema sababu kubwa ya timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri hadi sasa ni kutokana na washambuliaji kukosa umakini wa kutumia vyema nafasi wanazopata, huku akiweka wazi ugeni wake pia ni sababu nyingine.

Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya kikosi hicho kucheza michezo saba na kati ya hiyo kimetoka sare mitatu na kupoteza minne.

“Tunatengeneza sana nafasi ila umaliziaji umekuwa changamoto, kitendo ambacho kinatulazimu kufanya maboresho siku baada ya siku, bado tuna michezo mingi iliyo mbele yetu, hivyo tunaendelea kupambana ili kutatua hali hiyo,” alisema.

Ally aliongeza, changamoto nyingine ni kutozoea kufundisha soka la wanaume kwa muda mrefu kwani amekuwa akifundisha sana soka la wanawake, jambo ambalo kwake limempa mwanzo mgumu ingawa anaendelea kupata uzoefu ili kuzoea mazingira halisi.

Kocha huyo amejiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na JKT Queens aliyoitumikia kwa miaka minane tangu mwaka 2016, huku akiwahi pia kuifundisha JKT Kanembwa ya mkoani Kigoma kwa upande wa wanaume kwa msimu mmoja tu wa 2015-2016.

Related Posts