Dar es Salaam. Huenda siku chache zijazo, gari ndogo za abiria aina ya ‘Hiace’ zikaondolewa kabisa katikati ya miji mikubwa yote kufuatia utekelezaji wa mkakati maalumu wa kupunguza msongamano wa vyombo vya moto unaofanywa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).
Mkakati huo unalenga kuhakikisha leseni za kusafirisha abiria katika miji mikubwa zinazotolewa zinakuwa ni za magari makubwa badala ya hayo madogo.
Mbali na hilo, Latra pia imesema inaendelea kutoa elimu juu ya usafirishaji hasa kwa madereva wa bajaji katika maeneo mbalimbali nchini, ili kuhakikisha wanafuata kanuni hususani za ubebaji abiria kwa kuzingatia kiwango kilichowekwa.
Haya yalisemwa baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakazi wa mikoa tofauti ikiwemo Morogoro na Arusha ambapo wanadai kuendelea kuwapo kwa magari madogo ya abiria ni kutoendana na ukuaji wa miji.
“Arusha ni mji mkubwa, kuwapo kwa hivi vigari (hiace) ni fedheha, kwanza havikupi uhuru wa kukaa wala kusimama, haviendani na hadhi ya mji ulivyoku, ni vyema suala hili liangaliwe vizuri,” amesema Patrick Mushi mkazi wa Majengo mapya.
Maneno yake yanaungwa mkono na Janeth Masha ambaye ameiambia Mwananchi Digital kuwa uwepo wa vigari hivyo ni kushusha kiwango cha mji wa Arusha.
Malalamiko hayo pia yanatoka mkoani Morogoro ambapo wananchi wanataka hatua zichukuliwe ili gari hizo ndogo zisiingie mjini.
“Uwepo wake hata hadhi ya mkoa tu inapotea, sasa usiombe ukae siti ya karibu na mlangoni na mwingine akae mbele yako, mnaangaliana, mnapumuliana, mguu wake mmoja unapita katikati ya mguu wako si rafiki hili suala,” amesema Neema Salim mkazi wa Nanenane Morogoro.
Kufuatia suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Latra, Salum Pazzy ameiambia Mwananchi Digital kuwa tayari wameanza kutekeleza mpango maalumu wa kupunguza msongamano wa magari katikati ya miji kwa kuanzia jiji la Mwanza.
Kwa mujibu wake kinachofanyika ni kutotoa leseni mpya kwa gari ndogo za abiria na badala yake wanatoa leseni hizo kwa gari kubwa.
“Mwanza tumepunguza sana magari haya madogo, Arusha tumeanza kufanya uelimishaji kwa wadau wa usafirishaji na wakati mwingine tunawashauri waungane kuongeza nguvu ya mtaji ili waweze kuwa na vyombo vya kubeba abiria wengi,” amesema Pazzy.
Amesema muunganiko huo unafanywa kupitia chama cha kuweka na kukopa (Saccos) ili kuweka urahisi wa mashirikiano katika utoaji wa huduma.
“Wengi wanaelewa na kuona umuhimu wa kufanya hivi, ni mpango maalumu ambao ni endelevu,” amesema Pazzy.
Mbali na magari hayo madogo pia Latra imesema inafuatilia kwa ukaribu suala la usafirishaji wa abiria kwa kutumia bajaji katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha usimamizi wa sheria unazingatiwa.
Hiyo ni baada ya kuwapo kwa bajaji zinazobeba zaidi ya abiria watatu wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria. Pazzy anasema kwa kawaida bajaji haziruhusiwi kufanya kazi zinazofanywa na daladala na kuzidisha idadi kwa kiwango kinachotakiwa.
“Tunawaelimisha kwa kushirikiana na halmashauri za mkoa ambazo ndiyo zinahusika kupanga vituo kuhakikisha uzingatiwaji wa sheria unafanyika,” amesema Pazzy.
Awali Mwananchi ilifanya uchunguzi na kuangalia utendaji wa bajaji hizo katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dara es Salaam na kushuhudia ukiukwaji wa sheria ukifanyika.
Hali hii imekuwa ikitishia usalama wa abiria, hasa pale ambapo baadhi ya bajaji zimekuwa zikiongeza abiria hata kwenye kiti cha dereva.
Kitendo cha abiria kukaa mbele kunaweza kumsababishia dereva kukosa utulivu mzuri wa kukiongoza chombo jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa abiria wawapo safarini.
Akizungumza mmoja wa madereva wa bajaji, Ismail Shaban amesema mara nyingine wanalazimika kubeba abiria wengi kutokana na ufinyu wa vyombo vya moto.
“Mara nyingi wateja wanasisitiza kukaa wengi hasa wanapokuwa wana haraka au hawana pesa za kulipia bajaji mbili,” amesema Shabani.
John Mashauri ambaye pia ni dereva bajaji wa Mwenge jijini hapa, amesema kwa kawaida bajaji inaruhusiwa kubeba abiria watatu lakini kuna wakati wateja wanataka wabebe hata wanne au zaidi.
“Kwa upande wa kibiashara, tunapokataa tunaweza kupoteza mteja. Wengine wanaweza kusema watatafuta bajaji nyingine inayokubali kuwabeba wote, hivyo tunajikuta tunakubali ili kuepuka kupoteza kipato,”amesema John huku akiiomba Serikali kutoa elimu kwa abiria pamoja na semina kwa madereva
“Kwanza, elimu kwa abiria ni muhimu. Wengi hawajui madhara ya kubebwa zaidi ya uwezo wa bajaji, wanaona ni jambo la kawaida tu. Serikali au vyombo vya usalama barabarani vinapaswa kuhamasisha umma kuhusu hatari hizi. Pili, sisi madereva tunahitaji kupewa semina za mara kwa mara kuhusu usalama barabarani, na labda kuwe na ukaguzi mkali zaidi ili kuzuia hali hii.”
wakati madereva wakirusha lawama kwa abiria wenyewe wamekanusha wakisema idadi ya abiria kwenye bajaji huchochewa na dereva.
Philipo Edson amesema wakati mwingine madereva wamekuwa wakiwashawishi abiria kwa kuwapunguzia nauli wanapokuwa wengi.
“Wakati mwingine dereva anaweza kusema, mkiwa wengi nauli inakuwa nafuu na hiyo inatushawishi. Kwa hiyo tunakubali kwa sababu tutapunguza gharama za usafiri,” amesema Edson.
Hili linasemwa wakati ambao zipo kumbukumbu mbalimbali za ajali za bajaji ambazo zilikuwa zimebeba abiria wengi zikisababisha vifo na majeruhi.
Moja ya tukio lililowahi kushangaza wengi ni lile lililotokea Dodoma mwaka 2022 ambapo bajaji iliyokuwa imebeba abiria wanane kugongwa na gari ndogo ambapo watu watatu walifariki dunia na wengine kujeruhiwa.