Lori la chuo cha Mweka laua wanafunzi wawili

Tabora. Wanafunzi wawili wa Chuo cha Wanyamapori Mweka kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro, wamefariki dunia baada ya lori la chuo hicho walilokuwa wakisafiria kuelekea Inyonga mkoani Katavi kwenye mafunzo kwa vitendo kupata ajali.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Novemba 3, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema ajali hiyo imetokea jana usiku eneo la Tuli katika Manispaa ya Tabora.

Kamanda Abwao amesema lori hilo lilikuwa linawapeleka wanafunzi kwenye mafunzo kwa vitendo Inyonga mkoani Katavi.

Amesema katika ajali hiyo, wanafunzi wawili wamefariki dunia na wengine saba wamejeruhiwa.

“Tukio hili limetokea Novemba 2, 2024, saa 3:34 usiku katika eneo la Tuli, Barabara ya Tabora-Itigi wilayani Tabora. Lori lenye namba SU 41476 aina ya Camas, mali ya bodi ya Chuo cha Wanyamapori Mweka Moshi, likiendeshwa na dereva mwenye miaka 38, mkazi wa Moshi, lilikuwa safarini kutoka Moshi kuelekea Katavi kupitia Tabora na lilikuwa limebeba wanafunzi 40. Gari hilo lilitoka nje ya barabara na kupinduka na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja papo hapo, huku mwingine akifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete,” amesema kamanda huyo.

Amesema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva kutozingatia sheria jambo lililosababisha ajali hiyo na tayari dereva wa lori hilo anashikiliwa kwa ajili ya taratibu za kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria, ili hatua stahili zichukuliwe,” amesema Abwao.

Amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo ni pamoja na Evans David Lyimo na Ebenezer Benkras Isangya waliokuwa wakisoma stahahada ya usimamizi wanyamapori kwenye chuo hicho.

Hata hivyo, Abwao amewataka madereva wote hususan wa magari yanayobeba abiria kuchukua tahadhari kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali ambazo zinaweza kuepukika.

“Jeshi la Polisi tutaendelea kusimamia sheria na tutakuwa wakali zaidi kwa watakaokiuka sheria za usalama barabarani hususan kuelekea kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, niwatake watumiaji wazingatie sheria za usalama barabarani” amesema Abwao.

Kwa mujibu wa ripoti ya ‘Tanzania in Fugures’ ya mwaka 2023 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2023 jumla ya ajali 1,733 ziliripotiwa kutokea maeneo mbalimbali nchini

Ajali hizo kwa pamoja zilisababisha vifo vya watu 1,647 na kujeruhi 2,716.

Idadi ya waliojeruhiwa ilikuwa ni ongezeko kutoka 2,278 na waliokufa wakiwa 1,545 mwaka 2022 kutokana na ajali 1,720.

Related Posts