Ni watu wangapi wanatamani wangekuwa matajiri, kwa wale ambao si matajiri au ni matajiri lakini siyo matajiri wakubwa? Wangapi wanatamani kuoa au kuolewa na watu wenye mafanikio yawe kifedha, kielimu hata kimadaraka ambao ndiyo tunawaita matajiri? Bila shaka ni wengi.
Mafanikio au utajiri, una changamoto zake, hasa kutokana na wahusika wanavyojiona au wanavyoonekana kwa wengine. Pia, mafanikio ni dhana ambayo inaweza kuwa na maana nyingi.
Hivyo, hatutazama kwenye kuichambua au kuitafutia maana. Je, mafanikio hata maanguko yanaondoa utu wa mtu au kumbadili kuwa kitu kingine?
Je, ni watu wangapi wanaotoka kwenye familia maskini wakaoa au kuolewa na watu matajiri au wanaotoka kwenye familia maskini wakaoa au kuolewa kwenye familia zilizofanikiwa? Je, mafanikio ni nini na tunayapimaje?
Si rahisi kutoa majibu kwa maswali haya bila kujadili nini mtu binafsi anatafuta au kutaka. Tunachoweza kufanya hapa, ni kuangalia baadhi ya kesi zenye kutupa uzoefu ili katika kutafuta mwenza, mhusika ajue la kufanya au kutofanya.
Je, wakati wakitamani huu utajiri, waliwahi kujiuliza uhusiano wake na mafanikio katika mambo mengine muhimu katika maisha kama vile kupata watoto, ndoa bora, furaha, amani, ridhiko la moyo?
Japo huu hauchukuliwi kama utajiri kwa vile hauhusishi vitu anwai, vinaweza kuwa utajiri wa aina yake tena wenye thamani na umuhimu kuliko fedha au mali, madaraka, sifa na mambo mengine ya namna hii. Leo tutaongelea na kuunganisha mafanikio na ndoa.
Tutadurusu watu waliofanikiwa kuwa matajiri tena mabilionea duniani, au wenye madaraka makubwa duniani lakini wakashindwa katika taasisi ya ndoa.
Kama utajiri wa fedha ungekuwa ndiyo ufanisi katika ndoa, matajiri wakubwa wa dunia kama vile Bill Gates, Elon Musk, na Jeff Bizos wasingetaliki baada ya kushindwa ndoa.
Kama usomi ungekuwa ndiyo muhimili wa ndoa, wasomi wengi wasingeishi single pamoja na elimu na taaluma zao. Mapenzi hayana gwiji wa darasani, bali wa darasa liitwalo dunia litoalo uzoefu kama tunaotumia mbali na kujielimisha. Hakuna daktari wala profesa wa mapenzi.
Hata marais pamoja na kulindwa na kushauriwa sana mbali na kuogopewa kutokana na mamlaka yao, hawana mamlaka juu ya ndoa, vinginevyo marais au mawaziri wakuu kama Boris Johnson (Uingereza), Justin Trudeau (Canada), Silivio Berlusconi (Italia), Fredrik Reinfeldt (Sweden), Georgina Meloni (Italia) na marais kama vile Vladimir Putin (Urusi), Daniel arap Moi (Kenya) Fredrick Chiluba (Zambia), Donald Trump (Marekani), Nicholaus Sarkozy (Ufaransa), Hellen Johnson (Liberia), na Mary Banda (Malawi) wasingeachika na kuishia kuishi wapweke.
Hata hivyo, wapo watu waliofanikiwa katika yote, japo, kwa watu maarufu ni wachache. Kwa uzoefu tu tunawajua watu wachache wa namna hii kama vile bilionea Warren Buffett ambaye hata hivyo, pamoja na ubilionea wake, huishi maisha ya kawaida, kama hii ndiyo sababu ya kuonekana amefanikiwa katika utajiri na ndoa.
Pia, yupo Mark Zuckeberg na wengine wachache wakilinganishwa na walioshindwa katika taasisi hii.
Hivyo, hatutajifanya majaji wa kuhukumu, bali kutoa taaarifa kama chanzo na cheche vya wewe kufanya utafiti wako.
Japo hatujui sababu za kutofanikiwa kwa ndoa za wahusika hapo juu, tunaweza kujenga dhana mbalimbali, kama vile kuwa bize na mali, kuwa fahari kutokana na nguvu ya fedha au madaraka kiasi cha kuamini kuwa mhusika anaweza kumpata yeyote amtakaye.
Tunajenga hoja hizi kutokana na hisia kuwa watu waliofanikiwa huvutia zaidi ya wasiofanikiwa. Hivyo, hii hali pekee yaweza kuwa chanzo cha kukwama katika ndoa. Hii hutokana na kuweza kuzidiwa ushawishi hata mikakati ya wale wanaotaka kuoa au kuolewa na matajiri.
Wanaweza kujifanya kuwa yule ambaye siyo walivyo ili kupata fursa hii hasa wale wasaka ngawira, au kunyenyekea kwa muda ili waweze kupata wanachokitaka halafu wageuke na kurejea ule uhalisia wao.
Pia, mafanikio yanaweza kuwa kichaka cha watu wengine kujiona ni bora kuliko wale ambao hawajafanikiwa kama wao. Hivyo, kuyatumia kuwanyanyasa hata kuwatumia kama vifaa vyao kiasi cha kuwaacha pale wanapowachoka au wanapogundua kuwa kumbe walitumika kama chanzo cha mapato kwa wenzao kiasi cha kustuka na kuachana nao.
Pia, kupata wale ambao hawakuwategemea kinaweza kuwa chanzo cha kutofanikiwa kwa ndoa.Kwa machache tuliyodurusu hapo juu, unaweza kujitafutia mengine zaidi.
Hivyo, tunaweza kuhitimisha kuwa mafanikio ya aina moja yanaweza kuwa maanguko ya aina nyingine. Si ajabu. Kuna usemi kuwa Mungu hakupi vyote. Mwingine unasema, kila neema ina mitihani yake na kila mitahani yaweza kuwa na neema zake.