Mido achungulia dirisha dogo mapema

KIUNGO wa Cosmopolitan, Gilbert Boniface amesema moja ya malengo yake makubwa ni kuhakikisha anapambana ili kucheza Ligi Kuu Bara, wakati dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Desemba mwaka huu, kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya.

Nyota huyo aliyefunga bao moja msimu uliopita akiwa na kikosi hicho, alisema ni muda sasa wa kuangalia fursa mpya baada ya kucheza katika ligi za madaraja ya chini, japo hatoacha kujitoa kwa ajili ya timu hiyo kwenye kila mchezo wanaocheza.

“Nafikiri ni muda sahihi kwangu wa kuangalia na kupata changamoto mpya, naiheshimu Championship lakini nahitaji kuonekana zaidi na kutangaza kipaji changu, kwa sasa akili na mawazo yangu yapo Cosmopolitan kuhakikisha naipigania timu hapa ilipo.”

Akizungumzia msimu huu, Gilbert alisema umekuwa mgumu kutokana ushindani uliopo huku akiweka wazi timu hiyo angalau kwa sasa inaanza kujipata, baada ya kuanza vibaya huku akieleza kilichowakwamisha mwanzoni ni kutokuwa na muunganiko mzuri.

“Ligi imekuwa ngumu sana kwa sababu kila timu ina wachezaji bora na wazoefu, ukiangalia hapa kwetu wengi wetu ni wageni na hatujakaa pamoja kwa muda mrefu, michezo ya hivi karibuni inatupa mwanga ingawa tuna kazi kubwa ya kufanya pia.”

Related Posts