STRAIKA George Mpole ni kama amekata tamaa mapema kutokana na matokeo mabaya iliyonayo timu ya Pamba Jiji ambayo ndio pekee haijaonja ushindi Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa imecheza mechi 10, kufungwa tano na sare tano, akisema haoni kitu kitakachowaokoa kama sio kukaza buti.
Mpole amesema kama mchezaji anatamani kuondokana na jinamizi hilo, lakini halitawezekana kama kila mmoja ndani ya Pamba hatafunga kibwebwe na kukaza buti kwelikweli kwa mechi zilizosalia ili kuhakikisha wanajinusuru kurudi Ligi ya Championship.
Pamba iliyorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kuisotea kwa miaka 23 tangu pale iliposhuka, ina pointi tano ikishika nafasi ya 15 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo na mshambuliaji huyo wa zamani wa FC Lupopo, Mbeya City na Geita Gold alisema anatamani angalau wafunge mechi tatu mfululizo ili kurejesha morali ya upambanaji itakayoondoa upepo mbaya uliowaganda.
“Tukianza kushinda mechi kujiamini kutaongezeka, morali itakuwa juu, ndio maana tunaendelea kupambana na kuhamasishana hadi tutakapoanza kukaa katika mstari.
“Kwa upande wangu kama mshambuliaji napambana naona ni suala la muda kuanza kuhesabu mabao yangu. Sijawahi kukata tamaa na siyo mtu wa kukata tamaa ninapofanya jambo lolote,” aliongeza Mpole mwenye bao moja tu hadi sasa katika ligi ya msimu huu.
Mpole aliyemaliza na mabao 17 msimu wa 2021/22 Ligi Kuu Bara na kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora mbele ya Fiston Mayele aliyekuwa Yanga, alisema wakati anafunga mabao hayo akiwa Geita Gold hakuanza vizuri mechi za awali, lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda akaanza kutupia hadi akapata tuzo ya ufungaji bora.
“Me-chi bado zipo acha niendelee na mapambano. Najua huko mbele jina langu litatajwa kwa herufi kubwa,” alisema mchezaji huyo.