Maisha ni safari. Hivi ndivyo unaweza kumwelezea mtoto Antony Petro ambaye mwaka 2018 aliibua mijadala maeneo mbalimbali, hususan mitandaoni.
Video vya Antony wakati huo akiwa na umri wa miaka tisa, ilisambaa mitandaoni akimzuia baba yake, Petro Magogwa asiuze shamba la familia. Mtoto huyo hakuishia hapo, alikwenda kutoa taarifa polisi.
Antony ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ngundusi wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, alisema alizuia shamba hilo lisiuzwe ili yeye na ndugu zake wawili wa kike wasikose sehemu ya kuishi.
“Alitaka kuuza shamba ili sisi tukaishi wapi na tukalime wapi au tutatunzwa na nini? Niliamua kwenda polisi,” alisema Antony, Machi, 2018 katika mahojiano na Mwananchi, nyumbani kwao, Ngara.
Alipoulizwa kwa nini anaonekana ana akili nyingi, akijibu, “Mungu alinijaalia, kwa jinsi sina mama basi kanipa akili.”
Wadau mbalimbali walionyesha nia ya kumsaidia mtoto huyo ambaye wakati huo, Mwalimu Mkuu wa shule aliyokuwa anasoma ya Ngundusi, Josia Cleophace alisema hakuwa anafanya vizuri kitaaluma kutokana na mahudhurio yake darasani kuwa ya wastani.
Alisema mwanafunzi huyo alikuwa akienda kwenye vibanda vya wafanyabiashara kuomba misaada ili kupata chakula cha familia.
Miongoni mwa waliomsaidia mtoto huyo kwa hali na mali, ili kuhakikisha anafikia malengo yake ya kielimu ni Issihaka Msuya.
Msuya anasema aliamua kumsaidia mtoto huyo kwa kumpeleka Shule ya Msingi Aman Hills iliyopo Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro ambako aliendelea na masomo ya darasa la kwanza.
Antony amekuwa ni miongoni mwa maelfu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2024. Matokeo yaliyotangazwa Oktoba 30, 2024 na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) yanaonyesha mtoto huyo ni miongoni mwa waliofanya vizuri.
Katika matokeo hayo, Antony amefaulu kwa kupata daraja la A kwa maana masomo yote ya Kiswahili, Kiingereza, Maarifa, Hisabati, Sayansi na Uraia amepata alama A.
Yeye ni miongoni mwa wanafunzi sita kati ya 29 wa shule ya Aman Hills waliopata ufaulu wa alama A kwenye masomo yote.
Akizungumzia ufaulu wake huo, Antony ambaye sasa ana miaka 15, anasema anamshukuru Mungu kwa matokeo mazuri na hakutegemea kupata alama A kwenye masomo yake yote, jambo ambalo anasema ni mipango ya Mungu.
Anasema katika maisha yake anaamini unaweza kupambana na ukafanikiwa, hivyo yupo hapo kwa kuwa aliamini katika kupambana.
“Nafurahi kwa matokeo haya ambayo nimepata ufaulu mzuri, namshukuru Mungu kwa sababu sikutegemea kupata masomo zote A.
“Ukiamini kwamba unaweza na ukapambana unafanikiwa, nilipambana na ndio maana nimefikia hapa nilipo leo,” anasema Antony ambaye anazungumza vyema Kiingereza.
Akijibu swali aliloulizwa anatamani kuwa nani, Antony anasema, “Tangu nikiwa mdogo, nilitamani sana kuwa mwalimu ili niwafundishe watoto wafikie hatua ambayo nami nimefikia, hasa nije kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
‘Antony alijitambua’
Akimzungumzia mtoto huyo, Msuya aliyejitolea kumsaidia anasema historia ya kitaalamu kwa mtoto huyo ni ya kipekee kwa kuwa alijitambua mapema.
“Antony anajitambua alikotoka na siku zote anajua anatakiwa kujua anafanya nini, kwa hiyo amepata alama A zote kwenye mitihani yake, nampongeza sana na ninamfurahia mno kwamba ameweza kutimiza ndoto zake mpaka sasa.
“Kwa kuwa Antony amekuwa ‘inspiration’ kwenye jamii watu mbalimbali wanafuatilia kutoka katika mazingira magumu watakapofahamu Antony alikotoka itachochea watoto wengine kutokata tamaa na kujituma zaidi, naomba sana ombi hili lipokelewe na lichukuliwe kwa jicho la tofauti,” anasema.
Anasema mwishoni mwa mwaka 2017 kupitia mitandao ya kijamii aliona video yake ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii namna alivyopambana na baba yake asiuze shamba.
“Nilipoona ile video yake ikizunguka mtandaoni, nikatoa maoni yangu kwamba nitamsomesha, hivyo niko naye tangu kipindi hicho mpaka sasa amemaliza darasa la saba na hapa tupo kwenye shule yetu ya Furahini anajiandaa na masomo ya kidato cha kwanza mwakani,” anasema Msuya.
Anasema kwa sasa Antony amekuwa ni miongoni mwa watoto wa familia yake na wanaishi kama ndugu. “Antony ameubariki moyo wangu sana kwa sababu ameitendea haki nafasi aliyopewa kwa kuwa miongoni mwa watoto bora kitaaluma,”anasema Msuya.
Mwananchi limezungumza na baba mzazi, Petro ambaye anamshukuru Mungu kwa ufaulu wa mwanaye huyo na kwamba kama familia wanamtegea kwa kuwa amekuwa ni mpambanaji siku zote.
“Kwanza nimefurahi sana, nina mahali pakuishi na yote ni kwa sababu ya mwanangu Antony, namshukuru Antony maana yeye ndio baba yangu niseme hivyo, ninaamini atakuja kuwasaidia ndugu zake na wengine,” anasema Magogwa.
Akizungumzia mwanaye alivyokataa asiuze shamba la familia, Magogwa anasema kipindi hicho alikuwa anapitia wakati mgumu baada ya mkewe kufariki dunia na kumuacha na mtoto wa siku sita.
“Kipindi kile nilikuwa natafuta maisha yao, mama yao alifariki akaniachia watoto wadogo watatu, sasa wakati huo nikafikiria niwape nini, lakini nilipata aliyenipa fedha za kumtumza yule kichanga ambaye aliachwa na siku sita,” anasema.
“Hivyo ilitakiwa nipate fedha kwa ajili ya kununua maziwa, nilivyoona nina shamba la parachichi nikaona nikate kipande kidogo niuze, ili nipate maziwa ya mtoto na hawa wengine wadogo nilioachiwa, kuna mtu nilikuwa nimkatie shamba anipe Sh100,000 hadi Sh150,000 lengo ilikuwa nipate maziwa ya mtoto,” anasimulia Mzee Magogwa.
Editha, dada wa Antony anasema ufaulu wake umewafurahisha familia na kuwashangaza kwa kuwa kipindi Antony anakwenda Kilimanjaro alikuwa hajui kusoma wala kaandika kutokana na changamoto alizopitia.
“Kwa kweli tunashukuru Mungu, maana ni kitu ambacho tulikuwa hatutegemei kama atafanya vizuri kiasi hicho, kama dada yake nafurahi sana kwa matokeo haya, yeye ndio kichwa cha familia na ndiye tunayemtegemea,” anasema Editha.
Akizungumzia namna Antony alimzuia baba yake kuuza shamba, anasema licha ya kwamba baba yao alikuwa akiuza shamba la familia kutokana na matatizo, Antony alifanya vizuri kwa msimamo wake na kwamba leo hii wasingekuwa na mahali pakuishi.
“Mpaka sasa shamba lipo na halijauzwa, Antony alitupa msimamo japokuwa yeye aliondoka kusoma, lakini shamba lipo na bado tunapambana.”
‘Anaweza kuja kuwa kiongozi mzuri’
Diwani wa Kabanga, Hafidhi Abdallah anasema kwa maono ambayo Antony anayo na misimamo yake anaweza kuja kuwa kiongozi anayesimamia jambo na likafanikiwa.
“Kwa maono yake Antony na misimamo ile, baadaye anaweza kuja kuwa kiongozi anayeweza kusimamia kitu na kikafanyika, kikubwa aendelee kupambana,” anasema na kuongeza;
“Mtu ambaye ana uwezo wa kuthubutu kusimamia jambo na haki na ikapatikana ana kipaji kikubwa, naamini atakuja kufanya kitu cha maana katika kata yetu ya Kabanga au sehemu yoyote,” anasema.