Kuna mke wa mtu ananitaka na ananilazimisha sana, kwa muda niliokuwa karibu naye nimejikuta nampenda. Ila sitaki kuingia katika uhusiano naye kwa sababu ni mke wa mtu.
Kwa kuwa ninashindwa kuwa mbali naye, nifanyeje?
Unauchezea moto kwa mikono yako, bila shaka unaelekea kuungua. Umeshajua huyo ni mke wa mtu na ana nia mbaya ya kuisaliti ndoa yake na wewe unapanga kutumika kutimiza hilo.
Wahenga wameshawahi kusema mke wa mtu ni sumu, usidhani wanatania.
Muepuke huyo mwanamke, kama una namba yake ya simu ifute na umblock kabisa asikupate.
Acha mazoea na wake za watu, ni hatari kwa maisha yako, kwanza unaanzaje kuwa na mazoea na mke wa mtu.
Ninachokushauri fanya kila unachoweza uwe mbali naye kwa sababu mwisho wa siku utakayeumia ni wewe.
Utapoteza muda kuwa na mwanamke ambaye huwezi kumuoa, kuzaa naye, kufanya maisha kwa namna yoyote ile kwa sababu ni mke wa mtu.
Utapata raha na amani gani kuwa na mwanamke unayejificha ukiwa naye siku zote?
Ujauzito wa mke wangu unanitesa, sitaki mtoto mwingine
Mke wangu amebeba mimba sasa ina miezi miwili na wiki kadhaa, taabu na mateso ninayoyapata sijui kama nitakuja kumpa tena mimba mke wangu, kwani najuta.
Anti hata sijui kama na mwenzangu huko kwako unakuwa hivi, sina shida na kudai vitu ingawa vingine ninatakiwa nivilete hata sijui vinapatikana wapi.
Mke wangu amekuwa akitaka vitu vipya kabisa maishani mwangu, ukiachilia mbali kutonitaka kabisa nikanyage nyumbani na nikichelewa narushiwa chochote kilicho karibu, ninapata taabu ya kwenda masokoni kutafuta matunda mapya kabisa kuyasikia.
Juzijuzi nililazimika kwenda soko la Kisutu tena kwa kuelekezwa na wafanyakazi wenzangu kutafuta komamanga, kwa mara ya kwanza ndiyo nimeliona.
Akitaka kutapika kama nipo lazima hayo matapishi yatanifikia mwilini, atafanya kila hali, kisa anasema mimi ndiyo nimemsababishia haya yote.
Sitaki kukuambia kununa bila sababu, natamani watu wote waondoke hapo nyumbani tubaki wenyewe, nipe mbinu namna ya kuimaliza miezi saba iliyobaki, maana naona ninashindwa.
Kama kuna mambo yanafanywa na wanawake wajawazito yanaudhi hili ni mojawapo, hivi kuna ulazima gani kumtesa mtoto wa watu hata kama ndiyo amekupa hiyo mimba?
Najua baadhi ya mimba zina karaha, lakini wengine wanalazimisha na kuzidisha haya mambo.
Mara humpendi, mara umtapikie, mara unataka akakununulie vitu asivyovijua, huku ni kumkomoa.
Ninachojua ukiwa na mimba ndiyo umepata wakati wa kudeka kwa sababu unasikilizwa kila unalotaka, lakini ukizidisha vitimbi unaweza kumpoteza mumeo au mwenza wako mazima, kwani wengine huwa hawasamehe.
Tuache hizi, kama una changamoto mshirikishe, kama unamchukia mwambie taratibu kwani siyo vita na ninajua hii hali huwa inakwisha siyo ya kudumu.
Tuwape nafasi kina baba kufurahia matunda ya kile walichokifanya badala ya kukijutia.
Tukutane leba….