Rais Samia kufanya ziara ya siku tatu Cuba

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini Cuba kuanzia Novemba 6, 2024.

Jana Jumamosi, Novemba 2, 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliongoza kikao cha ujumbe wa Serikali ya Tanzania uliowasili Havana, Cuba kwa ajili ya maandalizi ya ziara hiyo.

Kikao hicho ni mwendelezo wa maandalizi ya ziara hiyo yaliyoanza na ukaguzi wa maeneo yatakayohusika wakati wa ziara ikiwamo  ukumbi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili na Bustani ya Mashujaa ‘Heroes Park’.

Ziara hiyo pamoja na mambo mengine, itaangazia zaidi ushirikiano wa nchi hizo mbili na changamoto za ulimwengu zinazohitaji suluhisho la pamoja kwa masilahi ya pande zote.

Pia, inalenga kuziwezesha Tanzania na Cuba kuendelea kukuza uhusiano wake wa kihistoria na kidiplomasia kuwa wa kimkakati kwa kufungua maeneo mapya ya ushirikiano yenye masilahi kiuchumi na kijamii.

Akiwa nchini humo Novemba 7,2024, Rais Samia anatarajia kufanya mazungumzo na mwenyeji wake

Rais wa Jamhuri ya Cuba, Miguel Díaz-Canel Bermudez. 

Vilevile, atapata wasaa wa kuweka shada la maua katika eneo la  kumbukumbu la José Martí Memorial ikiwa ni ishara ya kumuenzi shujaa huyo wa taifa la Cuba na kuzindua sanamu la hayati, Mwalimu Julius Nyerere katika eneo maalumu la mashujaa wa Afrika na waasisi wa mataifa lililopo jijini Havana.

Aidha, Rais Samia na Rais Bermúdez watashuhudia utiaji saini wa kumbukumbu za pamoja za ziara, hati ya makubaliano baina ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha Kikomunisti cha Cuba (CDC).

Novemba 8, 2024 Rais Samia atakuwa mgeni rasmi na kufungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili na baadaye viongozi hao watafanya ufunguzi rasmi wa kamusi ya Kispanyola na Kiswahili.

Pia watazindua kitabu cha maneno na misemo ya kila siku ya Kispanyola na Kiswahili kilichoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Havana,  ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa kati ya taasisi hizo Septemba, 2023.

Kongamano hilo ni sehemu ya jitihada zinazofanywa na ubalozi wa Tanzania nchini Cuba unaoongozwa na Balozi Humphrey Polepole.

Zikiwa na lengo la kutangaza utamaduni wa Mtanzania na lugha ya Kiswahili nchini humo, Ukanda wa Caribbean na Amerika ya Kusini. 

Kwa muktadha huo, Tanzania imejipambanua kukuza ushirikiano wake na Cuba katika maeneo ya afya, elimu, sanaa, michezo, utalii, lugha ya Kiswahili na kuvutia uwekezaji hususan katika eneo la uchumi wa buluu.

Related Posts