Rais wa Caf ashtakiwa Dar, kesi kunguruma kesho

KESI inayomhusisha bilionea wa Afrika Kusini na rais wa CAF, Patrice Motsepe na kampuni zake inatarajiwa kusikilizwa kesho, Jumatatu katika Divisheni ya Kibiashara ya Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Tanzania, Pula Group, imefungua kesi dhidi ya Motsepe na kampuni zake zikiwemo African Rainbow Minerals, African Rainbow Capital na ARCH Emerging Markets ikidai kuwa walivunja makubaliano ya kutoshindana walipowekeza katika kampuni ya Evolution Energy Minerals ya Australia, iliyoko karibu na mradi wa Pula’s graphite.

Kesi hiyo ilianza Oktoba 28, 2022, wakati Pula ilipowasilisha malalamiko Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kibiashara, ikidai uvunjaji wa makubaliano ya kutoshindana na yasiyo ya kufichua taarifa.

Hata hivyo, kesi hiyo yenye thamani ya dola 195 milioni  iliondolewa ghafla mwezi Mei 2023 kutokana na sababu za kiufundi. Rais wa Pula, Dk. Mary Stith, alitangaza Machi mwaka huu (2024) kwamba kesi hiyo iliwasilishwa upya mwezi Novemba 2023 na inasonga mbele.

“Kuondoa na kuwasilisha upya kesi kulifanywa kwa sababu za kiufundi. Tuna imani na hatua iliyopendekezwa na wanasheria wetu…,” alisema Dk. Stith katika taarifa yake ya Machi.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Charles Stith, alinukuliwa na Bloomberg akisema: “Kiwango hicho cha fidia kilitokana na tathmini ya chama cha tatu kuhusu hasara inayoweza kutokea kutokana na Motsepe na kampuni zake kuvunja makubaliano ya kutoshindana na yasiyo ya kufichua taarifa.”

Motsepe na kampuni zake wamekanusha madai ya uvunjaji wa makubaliano hayo na wamesema kuwa madai ya Pula hayana msingi wowote. Msemaji wa ARM alinukuliwa na Bloomberg akisema, “ARM ilikuwa inazingatia uwekezaji katika madini ambayo hawakuwa wameyachimba hapo awali wakati mradi wa Pula’s graphite ulipoletwa kwao. ARM walikubaliana na mkataba wa kutoshindana na Pula na baadaye wakaamua kutoendelea na uwekezaji huo, na walimjulisha Pula.”

Jaji Abdallah Gonzi anatarajiwa kutoa uamuzi kesho juu ya iwapo kesi kuu iendelee, huku maombi mengine kutoka kwa mdaiwa wa kwanza na wa pili yakisubiriwa, wakiomba marejeo ya kesi hiyo.

Pula inadai kuwa kulikuwepo na mkataba wa kutoshindana kwa kipindi cha miaka miwili, na kwamba kampuni za Motsepe zilifanya mazungumzo na kufikia makubaliano na kampuni ya Australia ndani ya kipindi hicho.

Stith, aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Tanzania, alisema kuwa uchunguzi mwingi wa madini nchini Tanzania unafanywa na kampuni za Australia na Canada, na kwamba mienendo isiyo ya haki ya kampuni kama ARM inaendeleza pengo kubwa katika sekta ya madini, jambo linalowadhuru Watanzania.

“Hali kama hiyo imekuwepo kote barani Afrika, na kesi hii inatarajiwa kutoa mwongozo wa kisheria wa kulinda haki za kampuni za ndani zinazoshindana na kampuni za kimataifa nchini Tanzania,” alisema.

Kesi hiyo inahusu makubaliano ya Julai 2019 kati ya Pula na ARM. Kulingana na mkataba huo, pande zote mbili zilikubaliana kwa muda wa miaka miwili kushiriki taarifa nyeti ambazo zingeliweka kampuni yoyote katika hali ya kushindwa endapo taarifa hizo zingetumika kushindana au kufikia makubaliano na mshindani mwingine.

Kutokana na makubaliano hayo, Pula ilishiriki taarifa zake za siri na wakurugenzi wakuu wa ARM kuhusu biashara ya uchimbaji madini na uwekezaji, ikiwemo maelezo ya shughuli za uchimbaji wa grafaiti huko Ruangwa, Tanzania, na ujuzi wa kitaalamu kuhusu akiba ya grafaiti ya Tanzania katika eneo hilo.

Kipengele muhimu cha mkataba huo kilikuwa ahadi ya kutoshindana wakati mkataba huo ukiwa bado una muda wa kutekelezwa. Pula inadai kuwa ARM walikiuka kipengele hicho cha kutoshindana kwa kuchelewesha utekelezaji na hatimaye kuamua kushirikiana na mshindani, Evolution, katika mradi wa Ruangwa.

Related Posts