Unguja. Imeelezwa kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inakabiliwa na tatizo la kiwango kidogo cha umeme kwenye laini zinazotoka Gridi ya Taifa ya Tanzania Bara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, John Kilangi amesema hayo leo Jumapili Novemba 3, 2024, katika kikao cha ushirikiano kilichofanyika Unguja, Zanzibar.
Kilangi amesema kituo cha kupokea umeme cha Mtoni kinapaswa kupokea kilovolti 132, lakini umeme unaofika ni kilovolti 110, hali inayosababisha baadhi ya vifaa kama transfoma kushindwa kufanya kazi ipasavyo.
Kilangi amesema changamoto hiyo hutokea hasa wakati kituo cha umeme cha Dar es Salaam kinapofanyiwa matengenezo.
Amesisitiza sekta ya nishati ni muhimu kwa uchumi na maendeleo ya nchi yoyote duniani, hivyo uwekezaji hauwezi kuendelea kama nishati hiyo ina changamoto.
Kilangi amesema Zanzibar kwa kiasi kikubwa inategemea sekta ya utalii katika maendeleo, hivyo bila ya kuwa na umeme imara, hata sekta hiyo itakwama.
“Naamini jambo hili litakuwa sehemu ya kulifanyia kazi kwa pande zote mbili ili kuona hatua za haraka tunazichukua katika kuondoa changamoto hii,” amesema Kilangi.
Mbali na umeme wa kawaida, kikao hicho pia kinajadili utekelezaji wa mpango mkuu wa kutumia nishati safi ya kupikia ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa muongozo wake na mkakati wa miaka 10 ambao umeshatangazwa.
Kilangi amesema kikao hicho pia kitajadili pia mipango mbalimbali ya kuimarisha utulivu wa gridi ya umeme, kuingia kwenye nishati mpya, uletaji wa gesi kutoka bara na kufanya tafiti mbalimbali ikiwamo tafiti za mawimbi, taka, upepo, jua na mawimbi ya bahari kwenye kuzalisha umeme.
“Watalaamu wetu watafanya tafiti kuona wapi katika maeneo hayo yanafaa katika uzalishaji wa umeme,” amesema.
Mbali na hayo, amesema upo mkakati unaofanywa kwa ajili ya joto la ardhi linalosaidia kuzalisha umeme kwa wingi iliyogundulika Kusini mwa Tanzania bara katika Mkoa wa Mtwara na kuna uwezekano wa kuzalisha karibu megawati 5000 na ukianza kuzalishwa hata Zanzibar itanufaika.
“Lengo letu ni kuona maeneo gani ya msingi ambayo tutayafanyia kazi na leo tutatengeneza mpango kazi wa mwaka mzima ikiwamo kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kuzalisha umeme, yote ni hayo ni kuona Zanzibar ina umeme wa uhakika,” amebainisha Kilangi.
Amesema ni imani yake kuwa vikao hivyo vitasaidia pia Zanzibar kuwa na vyanzo mbadala vya umeme bila ya kutegemea nishati hiyo kutoka gridi kubwa ya umeme ya Tanzania bara.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Tanzania, Felchesmi Mramba amesema wanafahamu kuwa Zanzibar imekuwa ikipata umeme mdogo kwa sababu ya kebo inayotoka bara kwenda Zanzibar imeanza kuzidiwa kutokana na matumizi ya Zanzibar kuongezeka.
Amesema kikao hicho kitajadili kuweka kebo ya tatu kutoka Dar es saalam kwenda Unguja ya kilovolti 220 na kebo nyingine kutokea Tanga kwenda Kisiwa cha Pemba yenye kilovolti 132.
Mramba amesema hatua mbalimbali za kuweka kebo hizo zimeshaanza ikiwamo kufanya upembuzi yakinifu chini ya bahari, kukamilisha mazungumzo ya benki ya maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kupata fedha za mkopo.
“Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) wameanza mpango wa ununuzi wa kumpata mshauri elekezi ambaye atasimamia mradi huo,” amesema Mramba.
Amesema kebo hizo zitabeba umeme mwingi ambao utawezesha Zanzibar kujitosheleza kwa nishati hiyo kwa miaka kadhaa ijayo.
Hata hivyo, amesema wizara hizo zipo sehemu zinategemeana ikiwamo Zanzibar kuchukua umeme kutoka bara, kwa hiyo mipango yoyote inayofanyika kwa upande huo kama isiporatibiwa vizuri na upande wa muungano basi upande mmoja unaweza kujikuta hauendi kwa kasi inayotakiwa.
Mbali na hayo amesema pia wanashirikiana kuendeleza miradi ikiwamo kushirikiana katika takwimu zitakazosaidia kuendelea miradi ya umeme wa jua, upepo, gesi na hata katika kushirikina katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
“Mambo haya yote tusipokaa pamoja na kuyafanyia kazi na kuyaratibu kwa pamoja inaweza kuwa vigumu kuweza kuona matokeo ambayo tunayoyatarajia,” amesisitiza.
Pia, amebainisha kuwa wizara hizo ni muhimu katika uchumi wa Tanzania, hivyo kupanga mipango ya pamoja inawasaidia kuendelea kwa haraka zaidi.
Ameahidi kuwa watahakikisha wanaendeleza ushirikiano kati ya pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuboresha huduma ambazo Serikali inatoa kupitia wizara hizo.