Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara mpya kwa kiwango cha lami.
Ili kuhakikisha barabara hizo zinadumu kwa kipindi kilichokusudiwa, mizani imewekwa katika maeneo ya kimkakati ili kudhibiti uharibifu unaosababishwa na magari ya mizigo yenye uzito wa kupita kiasi.
Kauli hizo zimetolewa na Meneja wa Kitengo cha Mizani cha Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Leonard Mombia, wakati akifunga mafunzo ya Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2018 kwa watumishi wa mizani na wasafirishaji wa Kanda ya Magharibi, inayojumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, na wenyeji Katavi.
Mhandisi Mombia amesema kuwa kuweka mizani ya kupima magari ni hatua muhimu ya kudhibiti uharibifu unaotokana na uzito wa ziada wa magari, hatua inayolenga kuhakikisha barabara zinadumu kwa muda mrefu na kuepusha serikali kuingia gharama kubwa za matengenezo, jambo ambalo linaathiri uchumi wa taifa.
“Ninawashukuru wasafirishaji na watumishi wa mizani wa mkoa wa Katavi kwa kushiriki kwa wingi katika mafunzo haya ya siku nne yaliyoanza tarehe 28 Oktoba 2024, yenye lengo la kuwajengea uwezo na kuwafanya wawe na weledi katika maeneo yao ya kazi. Mafunzo haya yamewapa uelewa wa pamoja juu ya sheria ya udhibiti wa uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018, pamoja na taratibu na miongozo mbalimbali, ili sekta ya usafirishaji iwe yenye tija na isiwe chanzo cha kuharibu barabara zetu,” alisema Mhandisi Mombia.
Ameendelea kwa kusema kuwa ni matarajio ya TANROADS kwamba washiriki wataendelea kuwa mabalozi wa kutekeleza sheria, taratibu, miongozo, na kanuni zinazolenga kulinda barabara dhidi ya athari zinazosababishwa na uzito wa magari ya mizigo, ili ziweze kudumu kwa kipindi kilichopangwa.
Aidha, amewahimiza wasafirishaji kutumia vizuri nafuu ya asilimia tano iliyotolewa na serikali kwa ajili ya kuhama mizigo kutoka kundi moja la mtambo kwenda jingine katika usafirishaji, na kuwashauri kuacha kutumia nafuu hiyo kwa ajili ya kubeba mzigo wa ziada.