Magu. Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) imemuua kiboko ambaye amekuwa msumbufu na kuhatarisha usalama wa wananchi wa Kijiji cha Ilungu, Kata ya Nyigogo, wilayani Magu Mkoa wa Mwanza.
Wananchi wa maeneo hayo kwa kipindi kirefu wamekuwa katika hali ya wasiwasi kutokana na kuwapo kwa mnyama huyo aliyeuawa leo Jumapili, Novemba 3, 2024 na nyama yake kugawiwa kwa wananchi hao kama kitoweo.
Askari wa Uhifadhi Mwandamizi kutoka Tawa, Loiruck Moses amesema wamefanikiwa kukabiliana na mnyama huyo ikiwa ni shughuli endelevu ya kuwadhibiti wanyama waharibifu.
Moses ametoa wito kwa wananchi pindi wanapokabiliana na wanyamapori wanapoonekana mahali popote watoe taarifa, ili askari wafike kukabiliana na wanyama hao.
Kwa upande wake, Ofisa Mifugo wa kata ya Nyigogo, Hamisa Gido amesema ni suala lililozoeleka katika maeneo mengi pindi mnyama kiboko anapouawa na nyama yake kupimwa na kuonekana haina dosari yoyote, hugawiwa kwa wananchi ili wapate kitoweo.
Mhifadhi Wanyama pori wilaya ya Magu, Christopher Christian amesema wanyamapori hao wamekuwa wasumbufu kwa wananchi wa kijiji hicho na wanaishukuru Tawa kwa kushirikiana pamoja kumdhibiti mnyama huyo.
Ofisa Mifugo wa kata hiyo ya Nyigogo, Hamis Gido amesema baada ya kudhibitisha kuwa nyama huyo ni salama kwa matumizi ya binadamu wamewapa wananchi ambao wameishukuru Serikali kwa kuwatatulia changamoto hiyo.
Mkazi wa eneo hilo, Pungwe Wilson ambaye pia ni mkulima amesema kwa muda mrefu wamekuwa na kilio kuhusu wanyama waharibifu wanaotokea Ziwa Victoria.
“Lakini sasa tunaishukuru Serikali kwa kumuua mnyama huyu ambaye pia amekuwa hatari hata kwa maisha yetu sisi wakulima,” amesema Wilson