VISA yamkwamisha Mbongo Uturuki | Mwanaspoti

MTANZANIA Hebron Shedrack anayekipiga Sisli Yeditepe inayoshiriki Ligi ya Walemavu nchini Uturuki amesema hajaondoka nchini hadi sasa kutokana na changamoto ya kibali cha kusafiria.

Nyota huyo anacheza ligi moja na Mtanzania mwenzake, Ramadhan Chomelo anayeitumikia klabu ya Konya.

Ligi ya nchi hiyo itaanza mwishoni mwa mwezi huu kutokana na mwingiliano wa ratiba ya michuano ya UEFA Champions League.

Shedrack alisema alipaswa tayari kuwapo klabuni lakini kutokana na changamoto ya VISA imemfanya hadi sasa kusalia Tanzania.

Aliongeza kuwa tayari kikosi cha timu hiyo kipo kambini kuanza maandalizi ya ligi na viongozi wa klabu hiyo wameingilia kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.

“Nilitakiwa niwe tayari klabuni na changamoto hiyo viongozi wangu wanaifahamu ndio maana wanapambana nipate kibali haraka ili niwahi, ni vitu vidogo tu, naamini ndani ya wiki hii nitafanikisha kwa kuwa pasipoti yangu iko ubalozini,” alisema Shedrack ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa na mabao manane na asisti 10.

Related Posts