Lindi. Ukosefu wa vitendea kazi na masoko ya uhakika ya zao la mwani ni changamoto zinazowakabili wajasiriamali na wakulima wa zao hilo mkoani Lindi, jambo linalowafanya wasinufaike nalo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Jumamosi Novemba 2, 2024 kwenye uzinduzi wa gulio la bidhaa za ushonaji na usindikaji na fursa za biashara, wakulima na wajasiriamali wa zao hilo, wameiomba Serikali iwasaidie kupata masoko ya mwani.
Mkulima wa mwani kutoka Wilaya ya Kilwa, Jakazi Ally amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kukosekana kwa soko na kukosa mashine ya kuchakatia mwani.
“Sisi wakulima na wajasiriamali wa zao la mwani, tunapata changamoto kubwa ya masoko ya mwani, tunauzia hapahapa, tunaiomba Serikali itusaidie kupata masoko ya uhakika ya zao la mwani pamoja na kutupatia mashine ya kuchakatia mwani,” amesema Ally.
Mkulima mwingine kutoka Manispaa ya Lindi, Zuhura Saidi amesema changamoto nyingine wanayoipata ni kukosekana kwa mashine ya kuchakatia mwani, jambo linalowafanya waende Dar es Salaam kufuata mashine ya mwani.
Amebainisha kwamba huko Dar es Salaam wanasaga kilo moja ya mwani kwa Sh5,000, hivyo ameiomba Serikali kuwapatia mashine na viwanda vya kuchakata mwani ili kuwapunguzia gharama.
“Sisi wajasiriamali na wakulima wa mwani tunatoka hapa Lindi hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kusaga mwani, tunatumia gharama kubwa sana, tunaiomba Serikali itusaidie kupata mashine pamoja na viwanda vya kuchakata mwani ili kupunguza gharama,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Bora Haule amesema wajasiriamali wa mkoani humo wanatumia fursa za uchumi wa buluu kuzalisha zao la mwani pamoja na mazao ya korosho na ufuta.
“Gulio hili ni kwa ajili ya wajasirimali kutumia fursa za uchumi wa buluu kwa kuzalisha zao la mwani pamoja na wajasiriamali wengine kuuza korosho na ufuta, na pia gulio hili litakuwa endelevu ambapo kila mwezi litafanyika mara mbili,” amesema Dk Haule.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amefikisha kilio cha wajasiriamali na wakulima hao kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Seleman Jafo akimwomba kuwapelekea viwanda vya kuchakata mwani na kiwanda cha kuchakata mafuta yanayotokana na zao la ufuta ili wazalishe bidhaa zao kwa urahisi zaidi.
“Nikuombe Waziri wa Viwanda na Biashara, utuletee viwanda vya kuchakata mwani, ufuta pamoja na viwanda vya kubangua zao la korosho ili wauze bidhaa zao ipasavyo kwani wajasiriamali wa Mkoa wa Lindi wanajishughulisha na bidhaa za viwanda.
“Pia, itasaidia bidhaa hizo kuuzwa hadi nje ya nchi kwani Mkoa wa Lindi unazalisha mwani na ufuta kwa wingi,” amesema mkuu huyo wa mkoa wa Lindi.
Baada ya kupokea maombi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Waziri Jafo amewataka Shirika la Viwanda vidogo vidogo (Sido) kuhakikisha wanajenga viwanda vidogo vya kuchakata mwani mkoani Lindi ili kutengeneza mwani uliosindikwa na kuwapa urahisi wajasiriamali hao.
Pia, amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha wanawapa nembo za ubora wajasiriamali ili kuwawezesha kuuza bidhaa zao kwa urahisi.
Waziri Jafo amesema viwanda vyote vilivyopo mikoa ya kusini vilivyokuwa vinatumika kubangua korosho vinakwenda kufufuliwa.
“Niwatake Sido kuhakikisha wanajenga viwanda vidogo vya mwani na watu wa TBS mhakikishe mnawapa wajasiriamali nembo za ubora ili wauze bidhaa zao kwa uhakika, na pia niwaambie kuwa viwanda vya kubangua korosho vilivyokuwa vinekufa kwa mikoa ya kusini vinakwenda kufufuliwa,” amesema Waziri Jafo.