Dar es Salaam. Mzimu wa kadi nyekundu unaonekana kutawala katika Uwanja wa Azam Complex kulinganisha na viwanja vingine vinavyotumika kwa Ligi Kuu msimu huu.
Idadi kubwa ya kadi nyekundu hadi sasa zimeonyeshwa katika Uwanja huo unaomilikiwa na Azam FC huku viwanja vingi vikiwa havijashuhudia kadi nyekundu hadi sasa.
Katika raundi 11 za Ligi Kuu msimu huu, idadi ya kadi nyekundu ambazo zimetolewa ni tano ambapo kati ya hizo, kadi nyekundu nne zimetolewa katika Uwanja wa Azam Complex na kadi nyekundu moja imetolewa katika Uwanja wa Kwaraa uliopo Babati.
Kadi nyekundu ya kwanza kutoka kwenye Uwanja wa Azam Complex ilikuwa ni Septemba 14 ambayo ilionyeshwa kwa Cheick Sidibe wa Azam FC aliyemfanyia faulo Salehe Masoud na mwamuzi aliyetoa kadi hiyo alikuwa ni Tatu Malogo.
Kadi ya pili kutolewa katika Uwanja huo ilikuwa ni ya Salehe Masoud huyohuyo wa Pamba aliyoipata Oktoba 3 dhidi ya Yanga kutoka kwa refa Sady Mrope baada ya kumfanyia faulo Chadrack Boka.
Oktoba 22, kipa Denis Richard wa JKT Tanzania alionyeshwa kadi nyekundu kwenye Uwanja huo wa Azam Complex na refa Ahmed Arajiga baada ya kufanya kosa la kugusa mpira kwa mikono nje ya eneo la hatari na kuzuia nafasi ya wazi ya bao la Yanga.
Juzi, Jumamosi, Refa Arajiga alimuonyesha kadi nyekundu Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga katika mchezo dhidi ya Azam FC, baada ya beki huyo kumchezea rafu, Nasso Saadun aliyekuwa akielekea kufunga.
Ukiondoa kadi hizo nne ambazo zimetolewa katika Uwanja wa Azam Complex, kadi nyekundu iliyotolewa katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati ilikuwa ni ya kiungo mshambuliaji wa KMC. Ibrahim Elias.