Azania yawaita Watanzania kuchangamkia hati fungani

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake, Benki ya Azania imewaita Watanzania kuchangamkia fursa ya ununuzi wa hatifungani (bondi) zake, ambapo kiasi cha chini itakuwa ni Sh500,000.

Hatifungani hiyo iliyopewa jina la “Bondi Yangu” inalenga kuuza hati fungani zenye thamani ya Sh30 bilioni ili kuiwezesha Azania kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali yenye malengo ya kimkakati kwenye sekta za uchumi zenye tija nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa hatifungani uliofanyika leo Jumatatu, Novemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Esther Mang’enya amesema utoaji wa hatifungani hiyo kwa umma unalenga kuongezea fedha na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za jamii na kuinua uchumi.

“Wawekezaji katika hatifungani ya Bondi Yangu watapata riba kubwa ya asilimia 12.5 kwa mwaka ambayo itatolewa kila baada ya miezi mitatu, huku ukomo wa kuwekeza katika Bondi Yangu ukiwa ni kipindi cha miaka minne, viwango hivi ni bora sana ukilinganisha na uwekezaji wa aina hii sokoni.’’ amesema Mang’enya.

Ofa hiyo itadumu kwa wiki nane kuanzia leo Jumatatu na baadaye hatifungani hiyo itaorodheshwa na kuuzwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), itakayomuwezesha mnunuzi wa hatifungani kuuza bondi yake kwa mnunuzi mwingine katika soko la upili kupitia madalali wa hisa walioidhinishwa na kupokea muhusika mkuu kabla ya tarehe ya ukomavu.

“Wanunuzi wa hatifungani hii ni watu binafsi, mashirika, hata kampuni. Lengo letu ni kukusanya Sh30 bilioni, lakini Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), wameturuhusu kufanya ongezeko la Sh15 bilioni, kwa hiyo tunaweza kwenda hadi Sh45 bilioni,” amesema Mang’enya.

Naye Mkurugenzi Mtendaji CMSA, Alfred Mkombo amesema hatua hiyo ni kubwa na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

“Bondi hii imekidhi matakwa ya kisheria kwa mujibu wa CMSA, kiasi cha kupewa idhini ya kuiingiza sokoni, hongereni sana Azania benki,” amesema Mkombo.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliungana na CMSA kwa kuwapongeza benki ya Azania kwa walichofanya kufanikisha jambo hili kubwa.

“Jukumu letu kama Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kuwaboreshea mazingira ya kufanya biashara ili mwisho wa siku muendelee kuja na ubunifu wenye tija kama huu. Hivyo nichukue nafasi hii kuwapongeza sana menejimenti na wafanyakazi wa benki hii ya Azania.”

Related Posts