Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wagombea walioenguliwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho za kuwania nafasi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, kuwa wavumilivu kwa kuwa wana nafasi nyingine ya udiwani katika uchaguzi mkuu mwakani.
Mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kuwania uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika Novemba 27, 2024 ulizua malalamiko, vurugu, madai ya kura feki kwa baadhi ya makada na wagombea walioenguliwa.
Baadhi ya mambo yaliyojitokeza ni wagombea walioshika nafasi ya kwanza kutopata uteuzi na badala yake walichukuliwa walioshika nafasi za mbili au mwisho, jambo lililolalamikiwa na makada walioshiriki mchakato huo.
Akizungumza na viongozi, wagombea waliopendekezwa na wasiopendekezwa Wilaya ya Kinondoni, leo Jumatatu Novemba 4, 2024, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema: “Mimi ni sehemu ya mfano mwaka 2020 sikuteuliwa, lakini nilishinda kura za maoni ila leo si mwenezi? Ningekuwa mbunge ningekuwa mwenezi? Kwa hiyo CCM inahitaji subira msiseme neno umekatwa, nyie hamkupendekezwa kugombea.”
“Niliongoza kura za maoni, sikuteuliwa na kamati kuweni na subira, nawatakia kila la heri waliokosa uvumilivu maana kabla ya uteuzi haujafanyika wakahamia upinzani kisha kurejea CCM, hamkuona nyie? akajibiwa na wanachama waliohudhuria mkutano huo kwamba waliwaona.”
Makalla amewataka makada wa CCM waliokosa uteuzi kuwa watulivu kwa kuwa kuna uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, wajipange upya kwa udiwani au uenyekiti wa tawi na kata kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho utakaofanyika 2027.
Makalla amesema chama hicho kinatoa pongezi kwa Wanaccm na viongozi kwa namna mchakato huo ulivyoendeshwa katika maeneo mbalimbali na wagombea waliojitokeza waliojitokeza walikuwa 500,000 na viongozi walioshikiri kura za maoni walikuwa milioni 10 nchi nzima.
“Tumefurahishwa na namna hamasa ilivyokuwapo na imevunja rekodi kuliko chaguzi zote za CCM. Imethibitika pasipo na shaka CCM ndio chama kikubwa kuliko chama kingine,” amesema Makalla.
Makalla amewaambia Watanzania kwamba, kura za maoni za CCM zimeshakamilika badala yake wawaunge mkono wagombea wa chama hicho, watakaosimamishwa akiwataka WanaCCM pia kuwa kitu kimoja.
Katika mkutano huo, Makalla amesema changamoto zote zilizojitokeza kwenye kura za maoni wanazifanyia kazi.
Amesema changamoto hizo ni chanya kwa chama kikubwa na yale yaliyokuwa ndani ya uwezo wao wameendelea kutatatua na sasa wanaenda kwenye uteuzi wa wagombea.
Aidha, chama hicho kimewataka wanachama wake kote nchini kuingia kwenye uchaguzi huo wakiwa wamoja, kufanya kampeni za kistaarabu ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi wa kishindo.
Katika hatua nyingine, Makalla amewataka Wanaccm kutobweteka katika maeneo watakayokuwa wagombea peke yao akisema hivi sasa hakuna kupita bila kupingwa badala yake wahakikishe wanapambana ili kuibuka kidedea.
“CCM imeweka wagombea kila kijiji, mtaa na vitongoji nchini, huwezi kushika dola kwa kusimamisha wagombea baadhi ya maeneo tu, ila chama hiki hakijaacha hata eneo moja kila mahali kuna watu,” amesema Makalla.
Jana, Jumapili Novemba 3, 2024 Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu alisema chama hicho, kimetoa maelekezo kwa ofisi katibu mkuu awasiliane na vyama vingine na wadau wa demokrasia kuandaa kampeni ya kuhamasisha umma kupiga kura ya hapana kwa wagombea wa CCM waliobaki peke yao.
Katika mkutano huo, Makalla, amesema mchakato wa kura za maoni kwa wagombea unaonesha utekelezaji wa demokrasia ndani ya chama hicho.
Amesema CCM imeonesha utaratibu wa kuwapata wagombea kwa njia ya demokrasia lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hawana demokrasia ya kuwapata wagombea ndani ya chama chao.
“Vyama vyao vinajiita vya kidemokrasia lakini mliona mahali walipiga kura za maoni ndani ya Chama cha Chadema? Waoneshe mahali walipotumia kigezo cha kuwakaba wagombea wao,” amehoji.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia kilichoelezwa na CCM, amesema walifuata utaratibu wa kuwateua wagombea wao na walifuata demokrasia ya wazi.
“Kwanza ni kauli ya uongo na kupotosha sisi tulifuata utaratibu wetu wa ndani wa kuwateua wagombea wetu, tulikuwa na demokrasia ya wazi ndio maana hakuna mahali wanachama wetu wanaondoka kwa sababu ya kunyimwa haki,” amesema Mrema.
Amesema wanachama wa CCM wamekuwa wakilalamika na kunukuliwa kwenye vyombo vya habari wamenyimwa haki na kura zao zimeendeshwa kwa rushwa na wengine wameondoka wamekuja kujiunga Chadema.
“Sisi hatukuwa na mizengwe kwenye chama chetu, aliyeshinda ndiye aliyetangazwa. Wapambane kwanza na mizengwe ndio waje waseme kuhusu Chadema,” amesisitiza.
Akizungumzia kuhusu kuwapokea wanachama wa CCM, amesema inatokana na wanavyolalamika kunyimwa haki na demokrasia ndani ya chama chao.
Mrema amesema wamesimamisha wagombea nchi nzima na hivi karibuni watatoa tathimini waliochukua na kurejesha fomu na watatoa taarifa kuhusu wagombea wao na mchakato mzima.